
Ofisi ya Rais wa Iran imekanusha vikali taarifa zinazosambaa zikidai kuwa Rais Massoud Pezeshkian amejiuzulu, ikizitaja kuwa ni za uongo na zisizo na msingi.
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Habari katika Ofisi ya Rais wa Iran, Mehdi Tabatabaei, kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, alisema madai hayo ni sehemu ya kampeni ya upotoshaji inayolenga kuvuruga umoja wa taifa.
“Muungano mbovu wa watu wenye msimamo mkali, waongo, wadanganyifu na wasiojali umelenga umoja mtakatifu na mshikamano wa kitaifa,” aliandika Tabatabaei.
Kauli hiyo imejibu taarifa zilizozagaa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii nchini Iran kufuatia matamshi ya mwanazuoni wa kidini Mohammad Bagher Kharrazi, ambaye anaripotiwa kuwa karibu na familia ya Kiongozi Mkuu wa Iran.
Kharrazi alidai kuwa Mojtaba Khamenei alisema kuwa iwapo Rais Pezeshkian angewasilisha tena ombi la kujiuzulu, basi lingekubaliwa.
Hata hivyo, hadi sasa Ofisi ya Rais wa Iran imesisitiza kuwa hakuna ukweli wowote kuhusu madai ya Rais Pezeshkian kujiuzulu na imewataka wananchi kupuuza taarifa zinazolenga kupotosha umma.