×

Mfalme wa Bernabeu Aendelea Kutawala, Vinicius Asaini Hadi 2032

Winga wa kimataifa wa Brazil, Vinicius Jr, amekubaliana na klabu ya Real Madrid kuongeza mkataba mpya wa miaka sita utakaomuweka Santiago Bernabeu hadi Juni 30, 2032.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alikuwa amebakiza mwaka mmoja pekee kwenye mkataba wake wa awali na alikuwa akihusishwa na kuhamia Arsenal, lakini sasa ameamua kuendelea na safari yake ndani ya klabu hiyo ya Hispania.

Real Madrid ilithibitisha makubaliano hayo, ikisema Vinicius Jr amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika kipindi cha mafanikio makubwa ya klabu hiyo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Vinicius aliandika:
“Miaka minane Bernabeu ni michache sana… Miaka sita zaidi, na kisha milele.”

Vinicius alijiunga na Real Madrid mwaka 2018 akitokea Flamengo ya Brazil na tangu hapo amekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Los Blancos.

Katika mechi 375 za mashindano yote akiwa na Real Madrid, Vinicius amefunga mabao 128, huku akiwa amefunga mabao 13 katika mechi 54 alizoichezea timu ya taifa ya Brazil.

Amesaidia Real Madrid kutwaa mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mataji matatu ya La Liga pamoja na Copa del Rey moja.

Mazungumzo ya mkataba mpya yalikuwa yamekwama kwa muda wa miezi 18 iliyopita, lakini ofa mpya kutoka kwa Real Madrid ilifanikisha makubaliano hayo.

Wakati huo huo, Arsenal ilikuwa tayari kuongeza juhudi za kumsajili Vinicius iwapo angekataa masharti ya Real Madrid, lakini sasa klabu hiyo ya England italazimika kuangalia chaguo jingine la mshambuliaji wa upande wa kushoto.

Kuongezwa kwa mkataba wa Vinicius kumekuja siku ambayo Real Madrid pia ilitangaza kumsajili winga wa Ivory Coast, Yan Diomande, kutoka RB Leipzig kwa ada inayoweza kufikia pauni milioni 120 (Sawa na Shilingi bilioni 408 za Tanzania)

Leave a Comment