
Dar es Salaam, Tanzania – Agosti 7, 2026: Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) imeipa Tanzania heshima kimataifa baada ya bidhaa zake nne kutunukiwa Gold Quality Awards 2026 na taasisi ya kimataifa ya tathmini ya ubora wa bidhaa, Monde Selection.
Bidhaa zilizotunukiwa tuzo hizo ni Serengeti Lite, Serengeti Lager, Serengeti Lemon pamoja na chapa ya vinywaji vikali ya TZEE.
Mafanikio hayo yamekuja wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Bia, huku SBL ikisema tuzo hizo ni uthibitisho wa ubora wa bidhaa zake na juhudi zinazoendelea katika kuboresha uzalishaji.
Tuzo za Gold Quality Awards hutolewa kwa bidhaa zinazofikia viwango vya juu vya ubora baada ya kupitia mchakato wa tathmini unaofanywa na wataalamu wa kimataifa. Bidhaa hutathminiwa kwa kuzingatia mambo mbalimbali, ikiwemo ubora, ladha, mwonekano, ubunifu, taarifa kwa mtumiaji na uzoefu wa mtumiaji.

Monde Selection ilianzishwa mwaka 1961 mjini Brussels, Ubelgiji, na imekuwa ikifanya tathmini ya bidhaa za walaji kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa zaidi ya miongo sita.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkurugenzi wa Ugavi wa SBL, Joseph Cheloti, amesema tuzo hizo ni uthibitisho wa dhamira ya kampuni hiyo katika kuhakikisha bidhaa zake zinaendelea kukidhi viwango vya kimataifa.
“Kupokea Tuzo za Gold Quality Awards kutoka Monde Selection ni heshima kubwa na uthibitisho kuwa bidhaa zetu zinakidhi viwango vya ubora vinavyotambulika kimataifa,” amesema Cheloti.
Amesema SBL itaendelea kuwekeza katika teknolojia, ubora, ubunifu na maendeleo ya bidhaa ili kuwapatia watumiaji bidhaa zinazokidhi viwango vya juu.
Kwa kutwaa tuzo nne za Gold Quality Awards kwa wakati mmoja, SBL imeendelea kujiongezea nafasi miongoni mwa wazalishaji wa vinywaji wanaotambulika kwa kuzingatia viwango vya ubora wa kimataifa.