
Dar es Salaam: Airtel Money kwa kushirikiana na Buni, Dar Teknohama Business Incubator (DTBI), Vocalize IoT Project na Techstar Innovation Hub, imeendesha mafunzo ya Internet of Things (IoT) na Digital Literacy kwa wanafunzi kutoka vyuo vikuu na VETA nchini.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea vijana uwezo wa kutumia teknolojia kubuni suluhisho zinazoweza kutatua changamoto mbalimbali za jamii, kuchochea ubunifu, kujiajiri na kuongeza fursa za ajira kupitia uchumi wa kidijitali.
Washiriki wamepata maarifa ya vitendo kuhusu matumizi ya IoT, namna ya kuunganisha teknolojia na huduma za kifedha za kidijitali pamoja na fursa zinazopatikana katika uchumi unaotegemea teknolojia.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Meneja wa Huduma za Kifedha, Miamala ya Kigeni na Majukwaa ya Kidijitali wa Airtel Money, Rita Nyamwehura, amesema kampuni hiyo inaendelea kuwawezesha Watanzania kutumia huduma za kidijitali na kuunga mkono jitihada za kuongeza matumizi ya mifumo ya malipo ya kielektroniki nchini.
Amesema vijana wanapaswa kutumia fursa zinazopatikana kupitia Airtel Money, ikiwemo kununua vifurushi, kulipa bili, kufanya malipo kupitia Lipa Namba pamoja na kutumia huduma nyingine za kifedha.
“Tunaamini teknolojia za kidijitali ni chachu ya ukuaji wa uchumi na fursa kwa vijana. Kupitia ushirikiano huu, tunataka kuwawezesha vijana kutumia ubunifu wao kutengeneza suluhisho zinazogusa maisha ya kila siku ya Watanzania,” amesema Nyamwehura.
Kwa upande wake, Business Development Manager wa JATEC, Elia Kinshaga, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwaandaa vijana kubuni teknolojia za IoT zinazoweza kutatua changamoto katika maeneo kama maji, usalama, usafirishaji, afya na utoaji wa huduma.
Ametolea mfano matumizi ya mita janja za maji zinazolipiwa kabla ya matumizi, akisema teknolojia hiyo inaweza kusaidia kupunguza upotevu wa mapato, kuongeza uwazi na kuboresha ufanisi wa huduma.
Kinshaga pia amesema kupitia ushirikiano kati ya Airtel na DTBI, zimeanzishwa Fursa Labs, zikiwa na vifaa vya TEHAMA, intaneti na maabara za ubunifu zinazowawezesha vijana kubuni, kujaribu na kukuza teknolojia zao.
Ameeleza kuwa moja ya matokeo ya maabara hizo ni mfumo wa Visomo unaomilikiwa na MagilaTech, ambao umewawezesha wanafunzi wa VETA kupata elimu kwa njia ya mtandao na sasa unatumiwa Tanzania pamoja na masoko ya kimataifa ikiwemo Dubai na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo wamesema wamepata uelewa zaidi kuhusu namna IoT inavyoweza kutumika kutatua changamoto za jamii na kuanzisha biashara zinazotumia teknolojia.
Mmoja wa washiriki, Levina Chifiye, mwanafunzi wa St. Joseph College of Engineering and Technology, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kuelewa matumizi ya IoT katika sekta za usalama, usafirishaji na mifumo ya malipo.
Ameongeza kuwa huduma za Airtel Money API zinaweza kuwapa wabunifu fursa ya kuunganisha mifumo ya malipo katika miradi yao ya kiteknolojia.