×

Binti wa Ruto Achumbiwa na Kijana wa Kitanzania, Wafanya Sherehe ya Jadi Intona Heritage Farm

Binti wa Rais wa Kenya, William Ruto, Charlene Ruto (kushoto), na Kulia ni kijana wa kitanzania Isaya Yunge.

Nairobi, Kenya. Binti wa Rais wa Kenya, William Ruto, Charlene Ruto, amefanya sherehe ya jadi ya “Koito ak Chaik”  leo Jumamosi, Agosti 8, 2026, katika eneo la Intona Heritage Farm, Kilgoris, Narok County, ikiwa ni sehemu ya mila za jamii ya Kalenjin kuelekea ndoa.

Sherehe hiyo imeweka rasmi katika uangalizi wa umma jina la mfanyabiashara Mtanzania mwenye umri wa miaka 36, Isaya Yunge, ambaye ametajwa kuwa mchumba wa Charlene.

Kwa jamii ya Kalenjin, Koito ni sherehe muhimu inayohusisha taratibu za uchumba na kuunganishwa kwa familia kabla ya ndoa. Tukio hilo la Charlene na Yunge limehudhuriwa na viongozi na wageni mbalimbali mashuhuri nchini Kenya.

Katika sherehe hiyo ya Koito, Charlene alionekana akiwa amevalia gauni la kahawia huku Yunge akiwa katika suti ya kahawia.

Wawili hao walishiriki pia katika ngoma za jadi za Kalenjin, huku eneo la sherehe likiwa limepambwa kwa vitambaa vya kijani na krimu.

Tukio hilo lilihudhuriwa na viongozi kadhaa wakubwa, akiwemo Naibu Rais wa Kenya Kithure Kindiki, Oburu Odinga, Mama Ida Odinga, Seneta Karen Nyamu na Mbunge Esther Passaris.

Wengine waliohudhuria ni Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen, Katibu Mkuu wa Hazina Chris Kiptoo, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja na Waziri wa Afya Aden Duale.

Baadhi ya wageni mashuhuri walifika kwa helikopta, huku sherehe ikiendelea kwa muziki, ngoma na mila za jamii ya Kalenjin.

Kwa muda mrefu, uhusiano wa Charlene na Yunge ulikuwa mbali na macho ya umma kabla ya taarifa za uchumba wao kuanza kujulikana.

Sasa, sherehe hiyo ya jadi imeweka wazi hatua mpya katika safari yao kuelekea ndoa, huku pia ikiongeza mjadala kuhusu uhusiano wa karibu unaoweza kujengwa kati ya familia mbili kutoka Kenya na Tanzania.

Lakini Yunge si jina jipya katika ulimwengu wa uongozi, teknolojia na kuwawezesha vijana kupata fursa.

Isaya Yunge ni nani?

Yunge ni mfanyabiashara na mtaalamu wa teknolojia kutoka Tanzania ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa SomaApps Technologies, kampuni iliyo nyuma ya SomaApp, jukwaa la kidijitali linalowaunganisha wanafunzi barani Afrika na fursa za elimu na ufadhili.

Kupitia SomaApp, zaidi ya vijana 7,000 barani Afrika wamepata msaada wa kufikia fursa za elimu, jambo lililomfanya Yunge kutambuliwa kwa kutumia teknolojia kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana katika kupata elimu.

Tuzo ya Malkia Elizabeth II

Mchango wake katika kuwawezesha vijana ulimletea Yunge Queen’s Young Leader Award mwaka 2018, tuzo iliyotolewa na Malkia Elizabeth II kwa vijana waliokuwa wakifanya kazi za kuleta mabadiliko katika jamii.

Yunge alikuwa miongoni mwa Watanzania wawili pekee waliotunukiwa tuzo hiyo mwaka huo.

Alianza uongozi akiwa kijana

Historia ya Yunge katika uongozi ilianza akiwa kijana.

Kati ya mwaka 2006 na 2007, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Tanzania’s Junior Council, akiwakilisha watoto katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa.

Baadaye, mwaka 2007 hadi 2008, alihudumu kama UNICEF African Youth Ambassador, akishiriki katika kampeni zinazohusu haki za watoto, mabadiliko ya tabianchi na ushiriki wa vijana katika kufanya maamuzi.

Mwaka 2007 pia alipata nafasi ya kimataifa baada ya kuwa kiongozi kijana kutoka Afrika aliyeshiriki kuhutubia Mkutano wa G8, akiwakilisha masuala na mitazamo ya vijana.

Safari yake katika biashara na teknolojia

Mbali na SomaApps Technologies, Yunge amewahi kushika nafasi ya Mkurugenzi na Mkurugenzi Mtendaji wa SPEKI Technologies kuanzia Januari 2022 hadi Julai 2023.

Katika nafasi hiyo, alihusika na ukuaji wa biashara, ubunifu na mabadiliko ya kimkakati ndani ya kampuni.

Ana elimu gani?

Yunge ana shahada ya Bachelor of Science in Insurance and Risk Management kutoka Institute of Finance Management (IFM) nchini Tanzania.

Pia amefanya masomo katika maeneo ya Economic Diplomacy na Digital Money, na baadaye akaendelea na mafunzo ya Leading Change in Entrepreneurship and Innovation katika University of Cambridge.

Leave a Comment