
Mwekezaji wa Simba na Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohammed Dewji, amewataka Wanasimba kuacha migawanyiko na malumbano, akisisitiza kuwa klabu hiyo si mali ya mtu mmoja bali ni ya Wanasimba wote.
Dewji ameyasema hayo leo, Agosti 8, 2026, wakati wa Tamasha la Simba Day lililofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Amesema katika kipindi ambacho Simba inapitia mabadiliko, ni muhimu kwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kuwa na umoja, kuuliza maswali na kutafuta ukweli badala ya kuamini kila taarifa inayosambaa.

“Naomba Wanasimba wenzangu, mnapoambiwa jambo, hoji, uliza na tafuta ukweli ni muhimu zaidi. Tusigawanyike. Simba haiwezi kujengwa kwa malumbano na migawanyiko. Kama tunataka kufika tunapolenga, tukamilishe mabadiliko haya na tusonge mbele pamoja,” amesema Dewji.
Amesema yuko tayari kuendelea kutekeleza wajibu wake katika maendeleo ya klabu hiyo, akisisitiza kuwa safari ya kuijenga Simba inahitaji ushirikiano wa kila Mwanasimba.

“Mimi niko tayari kufanya sehemu yangu, lakini Simba si ya mtu mmoja, Simba ni yetu sote. Safari tuliyoianza lazima tuihitimishwe,” amesema.
Bajeti ya Simba yafikia Sh bilioni 30
Katika hatua nyingine, Dewji amesema Simba imepiga hatua kubwa kifedha katika kipindi cha mabadiliko, akifichua kuwa bajeti ya klabu imeongezeka kutoka takribani Sh bilioni mbili kwa mwaka hadi kufikia takribani Sh bilioni 30 mwaka 2026.
Amesema ongezeko hilo ni sehemu ya mabadiliko makubwa yaliyofanyika ndani ya klabu kwa lengo la kuiwezesha Simba kushindana kwa kiwango cha juu zaidi.
“Katika kipindi hiki cha mabadiliko, tumepiga hatua kubwa. Bajeti ya klabu imeongezeka kutoka takribani shilingi bilioni mbili kwa mwaka hadi kufikia takribani shilingi bilioni 30 mwaka 2026. Tumepiga hatua na katika kipindi hiki tumefanya mabadiliko muhimu sana,” amesema.

Dewji ajibu wanaodai hatoi fedha Simba
Dewji pia amezungumzia madai mbalimbali yanayohusishwa na jina lake, ikiwemo tuhuma kwamba amekuwa hatoi fedha kwa klabu.
Amesema ameamua kukaa kimya dhidi ya baadhi ya kauli hizo kwa sababu anaamini maslahi ya Simba ni muhimu kuliko maslahi yake binafsi.
“Mengi yanasemwa kunihusu ambayo si ya kweli, lakini nimechagua kukaa kimya kwa sababu maslahi ya Simba ni makubwa kuliko maslahi yangu binafsi,” amesema.
Akizungumzia suala la kadi za wanachama, Dewji amesema madai kwamba yeye ndiye anayezizuia si sahihi, akieleza kuwa mchakato huo hauko chini ya upande wa mwekezaji.

“Wengine wanasema mimi nazuia kadi za wanachama. Ukweli ni kwamba kadi za wanachama hazijatolewa na upande wa mwekezaji. Wanasimba wanaambiwa hivyo na badala ya kuhoji, wengine wanaamini,” amesema.
Kuhusu madai kwamba mwekezaji hatoi fedha, Dewji amesema amekuwa akiendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuziba mapengo mbalimbali na kutekeleza wajibu wake ili kuhakikisha klabu inaendelea kusonga mbele.
“Wapo pia wanaosema mwekezaji hatoi fedha, lakini ukweli ni kwamba nimeendelea kutoa fedha kuziba mapengo mengi na kutekeleza wajibu wangu ili kuifanya Simba isonge mbele,” amesema.
Kauli za Dewji zimekuja wakati Simba ikiendelea na mchakato wa mabadiliko ndani ya klabu, huku akisisitiza umuhimu wa umoja na ushirikiano wa Wanasimba katika safari ya kufikia malengo ya klabu hiyo.