
Rais wa FIFA, Gianni Infantino, amekanusha vikali madai kwamba UEFA ilimlipa kiasi kikubwa cha fedha mwanamke anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi naye wakati alipokuwa Katibu Mkuu wa UEFA.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliochapishwa na The Daily Telegraph, mwanamke huyo alidaiwa kupewa malipo ya kuondoka kazini (severance payment) na UEFA kufuatia uhusiano huo uliodaiwa kutokea kipindi ambacho Infantino alikuwa akiongoza shughuli za kila siku za UEFA.
Infantino, ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa UEFA kuanzia mwaka 2009 hadi 2016, kupitia msemaji wake amekanusha madai hayo akisema ni “yasiyo ya kweli kabisa”.
“Gianni Infantino anakataa vikali madai haya, ambayo hayana ukweli wowote,” msemaji wake aliiambia The Telegraph.
Msemaji huyo pia alisema kuwa madai yoyote yanayodokeza kwamba Infantino alijihusisha na tabia isiyofaa au kuvunja kanuni ni ya kumchafulia jina.
UEFA yakiri kufanya malipo
Hata hivyo, UEFA imethibitisha kuwa ilifanya malipo kwa mwanamke huyo, ingawa imekanusha kwamba malipo hayo yalikuwa kinyume cha kanuni zilizokuwepo wakati huo.
Kwa mujibu wa UEFA, malipo hayo yalihusisha gharama za mwanamke huyo kusoma MBA katika shule ya biashara ya eneo hilo.
UEFA imesema malipo yote yalifanyika kwa kuzingatia kanuni zilizokuwa zikitumika wakati huo.
Hata hivyo, taasisi hiyo imeongeza kuwa kanuni zake zimeimarishwa tangu wakati huo ili kuendana na viwango vya taasisi kubwa na yenye hadhi ya kimataifa.
Madai hayo yanaibuka wakati ambao Infantino anakabiliwa na presha kuhusu mustakabali wake kama rais wa FIFA, kufuatia mpango wake uliokwama wa kuuza sehemu ya haki za kibiashara za Kombe la Dunia kwa wawekezaji binafsi.