SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeeleza kuwa ofa ya vifaa vya intaneti iliyokuwa ikitolewa wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima ya Nane Nane itaendelea hata baada ya maonesho hayo kumalizika.
Akizungumza jijini Dodoma baada ya kufungwa kwa maonesho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni, Afisa Mahusiano Mwandamizi wa TTCL, Debora Ngalima, amesema wananchi wataendelea kunufaika na ofa hiyo kupitia vituo na maduka ya shirika hilo yaliyopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Ngalima, maonesho ya Nane Nane yalikuwa fursa muhimu kwa TTCL kuwafikia wananchi na kuwapatia taarifa kuhusu huduma mbalimbali za mawasiliano zinazotolewa na shirika hilo.
Amesema wananchi waliotembelea banda la TTCL walipata fursa ya kufahamu huduma mbalimbali, ikiwemo huduma za intaneti na vifaa vinavyowawezesha kuendelea kuwa connected katika shughuli zao za kila siku.
“Tunawashukuru wananchi wote kwa kutembelea banda letu katika maonesho haya ya Nane Nane. Pamoja na maonesho kufikia tamati, ofa katika vifaa vya intaneti itaendelea kama kawaida,” amesema Ngalima.
Ameongeza kuwa wananchi wanaohitaji vifaa na huduma za intaneti za TTCL wanaweza kuendelea kufika katika vituo na maduka ya shirika hilo vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata fursa ya kutumia huduma za intaneti na vifaa vya mawasiliano hata baada ya kumalizika kwa Maonesho ya Nane Nane.
