×

Simba Day Yaanza Kwa Kishindo, Wanamsimba Wakataa Kukaa Chini (Picha +Video)

Leo, Agosti 8, 2026, Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam limegeuka kuwa uwanja wa shangwe, huku maelfu ya mashabiki wa Simba wakijitokeza kwa wingi kushiriki tamasha la Simba Day.

Hali ya hewa ya Simba Day imepamba moto tangu mapema, huku mashabiki wakiwa katika shamrashamra, nyimbo na burudani mbalimbali wakisubiri kwa hamu matukio makubwa ya siku hiyo.

Burudani imechukua nafasi kubwa, ambapo DJ Sinyorita amekuwa akiongoza burudani na kuwafanya mashabiki wa Simba kuimba, kucheza na kuonyesha mapenzi yao kwa klabu hiyo.

Mbali na burudani, Simba Day 2026 ni sehemu muhimu ya maandalizi ya klabu kuelekea msimu wa 2026/2027, ambapo Simba inatarajiwa kuwatambulisha rasmi wachezaji wake pamoja na benchi la ufundi litakalokuwa likiongoza kikosi hicho.

Baada ya hafla hiyo, mashabiki watapata nafasi ya kumuona Simba ikipimana nguvu na Kenya Police katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaohitimisha shughuli za siku hiyo.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya kikosi, huku mashabiki wakitamani kuona uwezo wa nyota wapya na mwelekeo wa timu kuelekea msimu mpya.

Kwa sasa, Uwanja wa Uhuru ni burudani tupu — Wanamsimbazi wamejaa, muziki unadunda na hamasa imepanda juu.

Simba Day 2026: Siku ya Mnyama, siku ya Wanamsimbazi! 

Mwanaisha Akida almaarufu kama Dj Sinyorita.

Leave a Comment