×

Wakulima Nyanda za Juu Kusini Wapokea Malipo ya Mazao Kupitia Simu

Mbeya. Wakulima katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wameendelea kunufaika na huduma za malipo ya kidijitali zinazotolewa na Mixx by Yas, zinazowawezesha kupokea fedha za mauzo ya mazao moja kwa moja kupitia simu zao, hivyo kupunguza ulazima wa kusafiri umbali mrefu kufuatilia malipo.

Huduma hizo zimekuwa na umuhimu kwa wakulima waliopo maeneo ya vijijini na mbali na taasisi za kifedha, kwa kuwapatia njia rahisi na salama ya kupokea na kufuatilia fedha baada ya kuuza mazao yao.

Akizungumza wakati wa kilele cha Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Meneja wa Biashara wa Mixx by Yas Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Charles Gardner, alisema matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali yanaendelea kupunguza baadhi ya changamoto ambazo wakulima wamekuwa wakikumbana nazo katika kupokea fedha za mazao.

Gardner alisema kupitia Mixx by Yas, mkulima anaweza kupokea malipo moja kwa moja kwenye simu yake bila kulazimika kusafiri kwenda kufuata fedha, hatua inayookoa muda na gharama na kupunguza utegemezi wa fedha taslimu.
“Tunataka mkulima aweze kupokea fedha za mazao yake kwa urahisi popote alipo. Badala ya kutumia muda na gharama kusafiri kufuatilia malipo, fedha zinaweza kumfikia moja kwa moja kupitia simu yake na akazitumia kulingana na mahitaji yake,” alisema Gardner.

Alisema Mixx by Yas inaendelea kutumia Maonesho ya Nanenane kama jukwaa la kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali na namna zinavyoweza kurahisisha shughuli zao za kila siku.

Baadhi ya wakulima wanaotumia huduma hizo wamesema malipo kupitia simu yamepunguza muda waliokuwa wakitumia kusubiri au kufuatilia fedha baada ya kuuza mazao yao.

Joyce Mube, mkulima kutoka Tunduma, alisema mfumo huo umemrahisishia kupokea na kufuatilia malipo ya mazao yake bila kulazimika kusafiri kwenda kufuata fedha.
“Unapopokea fedha kupitia simu unakuwa na uhakika wa malipo yako na unaweza kuyafuatilia kwa urahisi. Pia inapunguza muda na gharama ambazo tungetumia kwenda kufuata fedha,” alisema Mube.

Wakati huohuo, Meneja wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Roodny Alananga, amewataka wakulima na wajasiriamali kuzingatia ubora na viwango vya bidhaa zao ili kuongeza ushindani na kupata fursa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Alananga alisema elimu inayotolewa na TBS inalenga kuwasaidia wakulima na wajasiriamali kuboresha bidhaa zao na kuhakikisha zinakidhi viwango vinavyohitajika katika masoko mbalimbali.

Maonesho ya Nanenane yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa wakulima kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo na kupata taarifa kuhusu teknolojia, huduma za kifedha, masoko na viwango vya bidhaa vinavyoweza kusaidia kuongeza tija na kipato.

MWISHO

Leave a Comment