×

Airtel Yatoa Elimu ya Usalama wa Mtandao Nane Nane, Yawaonya Wananchi Dhidi ya Matapeli

Dodoma, Agosti 8, 2026 — Kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usalama wa mtandao na namna ya kujikinga na matapeli wa kidijitali kupitia Maonesho ya Wakulima ya Nane Nane yanayoendelea katika mikoa mbalimbali nchini.

Airtel imeshiriki katika maonesho hayo yanayofanyika Dodoma, Morogoro, Arusha, Mbeya, Rukwa, Mwanza na Tabora, huku ikitumia fursa hiyo kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi salama ya huduma za kidijitali pamoja na kusogeza huduma zake karibu na wateja.

Katika maonesho hayo, Airtel pia inaendelea na kampeni yake ya “Minyoosho Inaendelea”, inayowahamasisha wateja kutumia huduma za kidijitali kufanya miamala kupitia My Airtel App pamoja na huduma mbalimbali za Airtel Money kwa urahisi, haraka na kwa usalama.

Akizungumza katika Maonesho ya Nane Nane, Meneja wa Biashara wa Airtel Mkoa wa Dodoma, Salum Juma Ngululu, amesema ushiriki wa kampuni hiyo ni sehemu ya dhamira ya kuwa karibu na wateja huku ikiwapatia elimu kuhusu matumizi salama ya teknolojia.

Ngululu amesema elimu hiyo ni muhimu kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kidijitali na miamala ya kifedha kupitia simu, hali inayowafanya wananchi kuwa katika hatari ya kukutana na watu wanaotumia njia mbalimbali za mawasiliano kuwalaghai au kuwaibia taarifa zao.

Amesisitiza kuwa wateja wanapaswa kulinda taarifa zao binafsi na za kifedha, ikiwemo PIN ya Airtel Money, OTP, nenosiri na taarifa nyingine za siri, na kutomkabidhi mtu mwingine taarifa hizo kwa kisingizio chochote.

“Tunawahimiza wateja kuwa makini wanapopokea simu, ujumbe au mawasiliano kutoka kwa watu wasiofahamika wanaodai kuwa wawakilishi wa Airtel. Mteja hapaswi kutoa taarifa zake za siri, na anapaswa kutumia njia rasmi za Airtel anapokuwa na mashaka au anapohitaji msaada kuhusu huduma zake,” amesema Ngululu.

Airtel Yaendelea na Kampeni ya “Minyoosho Inaendelea”

Akizungumzia kampeni ya “Minyoosho Inaendelea”, Ngululu amesema inalenga kuongeza matumizi ya huduma za kidijitali kwa kuwahamasisha wateja kutumia My Airtel App kufanya miamala yao ya kila siku ya Airtel Money kwa njia rahisi na salama.

Kupitia kampeni hiyo, wateja wanaotumia My Airtel App kufanya miamala inayokidhi vigezo wanapata fursa ya kushiriki katika mchezo wa Spin & Win na kujishindia zawadi.

Kwa mujibu wa Ngululu, kampeni hiyo inalenga pia kuhamasisha wananchi kuongeza matumizi ya huduma za kidijitali katika shughuli zao za kila siku.

Amesema kampeni hiyo inaendana na dira ya Airtel ya “Kila Kona”, inayolenga kuhakikisha huduma za mawasiliano na kidijitali zinawafikia Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, ushiriki wa Airtel katika Maonesho ya Nane Nane unalenga kuwawezesha wananchi kupata huduma moja kwa moja katika mabanda ya kampuni hiyo, huku wakipata maelezo kuhusu bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa.

Airtel imesema itaendelea kutumia majukwaa kama Maonesho ya Nane Nane kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi salama ya teknolojia na kuwawezesha kutumia huduma za kidijitali kwa ufanisi zaidi.

Leave a Comment