×

Lissu Aibua Maswali Kuhusu Ushahidi wa Video Katika Kesi ya Uhaini

IKIWA ni mwendelezo wa maswali ya dodoso kwa ACP Amini Mahamba, shahidi wa 16 katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, Lissu amemhoji shahidi kuhusu madai kwamba yeye ndiye aliyechapisha na kusambaza video ya mkutano wa CHADEMA kwenye YouTube ya Jambo TV.

Katika mahojiano hayo, Lissu alimbana shahidi kuhusu ushahidi unaothibitisha kuwa ndiye aliyechapisha video hiyo, huku shahidi akikiri kutokuwa na uhakika kama Lissu ni mfanyakazi, mpiga picha, mtangazaji au ana nywila ya kuingia kwenye mtandao wa Jambo TV. Shahidi pia alikiri kuwa katika maelezo ya mashahidi P na P1, walieleza kuwa wao ndio waliorekodi na kurusha mubashara mkutano huo kupitia Jambo TV.

Tundu Lissu aliendelea kumuuliza shahidi kuhusu uchunguzi uliofanyika katika makao makuu ya CHADEMA, ambapo shahidi alikiri kuwa hakuwahoji baadhi ya viongozi wa chama kuhusu mwaliko na mkutano huo. Aidha, shahidi alikiri kwamba Lissu, kama Mwenyekiti wa CHADEMA, hawajibiki kijinai kwa makosa yanayofanywa na viongozi wenzake.

Katika sehemu nyingine ya dodoso, Lissu alihoji msingi wa madai ya uhaini akihusianisha hotuba yake na masuala ya uchaguzi. Shahidi alikiri kuwa Katiba haijaainisha kuvuruga uchaguzi kama kosa la uhaini.

Lissu pia alibainisha kuwa katika maneno yanayodaiwa kuwa ya uhaini hakutaja Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Philip Mpango, Waziri Mkuu wa zamani Kassim Majaliwa wala Tume ya Uchaguzi. Akimhoji shahidi kuhusu sababu ya yeye kushikiliwa wakati ushahidi unaonyesha kuwa P na P1 ndio waliorusha video hiyo, Lissu alisema: “Mwaka mmoja na miezi minne gerezani sio mateso.”

Leave a Comment