×

Kesi Ya Mauaji Ya Tupac Shakur Yaanza Kusikilizwa Rasmi

Kesi ya kihistoria inayohusiana na mauaji ya nyota maarufu wa muziki wa Hip-Hop, Tupac Shakur, imeanza rasmi katika Mahakama ya Wilaya ya Clark County, jijini Las Vegas, Marekani, ikiwa ni karibu miaka 30 tangu mauaji hayo  yaliyotikisa dunia nzima ya burudani.

Mshtakiwa katika kesi hii ni Duane “Keffe D” Davis, mwenye umri wa miaka 63, aliyekuwa kiongozi wa genge la kihalifu la South Side Compton Crips. Davis ndiye mtu wa kwanza na pekee kufikishwa mahakamani kwa kuhusiana  na mauaji ya Shakur, yaliyotokea Septemba 7, 1996, wakati akiwa Las Vegas baada ya kutazama mchezo wa ndondi kati ya Mike Tyson na Bruce Seldon.

Uteuzi wa jopo la majaji 12 pamoja na wasaidizi wanne ulikamilika Jumatano, Agosti 12, 2026, baada ya siku nne za mahojiano yaliyohusisha zaidi ya wakazi 100 wa Clark County. Hoja za ufunguzi zilitolewa rasmi Jumatatu, Agosti 17, 2026, ambapo mwendesha mashtaka mkuu, Binu Palal, alieleza mahakama kuwa Davis alipanga na kuratibu shambulizi hilo kwa nia ya kulipiza kisasi, baada ya mpwa wake, Orlando Anderson, kupigwa na kudhalilishwa na kundi la Tupac usiku huo huo katika hoteli ya MGM Grand.

Siku ya kwanza ya Ushahidi, ilishuhudia mashahidi wanne wakitoa maelezo yao mbele ya jopo la mahakimu, wakiwemo Garry Dale, aliyekuwa ofisa wa polisi wa Las Vegas Metropolitan  akifanya doria kwa baiskeli usiku wa tukio, na James McDonald, aliyekuwa mkuu wa ulinzi katika klabu ya usiku ya Club 662, ambapo Shakur na msafara wake walikuwa wakielekea kabla ya kushambuliwa.

Ushahidi huo unatarajiwa kuendelea leo Jumanne, Agosti 18, 2026, huku Jaji Carli Kierny, anayesimamia shauri hilo, akitarajia kesi hiyo kudumu kwa wiki kadhaa.

Ushahidi mkuu unaotumiwa na upande wa mashtaka dhidi ya Davis ni kitabu chake mwenyewe, “Compton Street Legend,” alichokiandika mwaka 2019, ambapo alieleza kwa kina mchango wake katika tukio hilo.

Wakili wa utetezi wa Davis, Michael Sanft, amehoji uaminifu wa wapelelezi waliohuskika na uchunguzi wa awali, akisisitiza kuwa upande wa mashtaka hautaweza kumhusisha moja kwa moja Davis na risasi zilizomuua Shakur.

Ni muhimu kufahamu kuwa Davis hajawahi kudaiwa kuwa ndiye aliyefyatua risasi hizo, bali anahusishwa kama mpangaji na muratibu mkuu wa shambulizi hilo.

Miongoni mwa watu wanaotarajiwa kuitwa mahakamani wiki zijazo ni Marion “Suge” Knight, aliyekuwa Bosi wa kampuni ya Death Row Records na alikuwa akiendesha gari alilokuwamo Shakur usiku wa mauaji; Greg Kading, aliyekuwa ofisa wa polisi wa Los Angeles aliyeandika kitabu kinachomhusisha Davis na mauaji hayo; Gavana wa sasa wa Nevada, Joe Lombardo, ambaye alikuwa Meya wa zamani wa Clark County; na ,Vegas, Oscar Goodman.

Davis anakabiliwa na shtaka la mauaji kwa kutumia silaha hatari, akihusishwa na kukuza shughuli za genge la kihalifu, amekana mashtaka yote dhidi yake.

Endapo atapatikana na hatia, anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha jela bila uwezekano wa kuachiliwa kwa msamaha, hukumu itakayofunga rasmi mojawapo ya mafumbo makubwa zaidi ya utamaduni wa muziki wa Hip-Hop katika historia.

Stori na Mathna Ramadhani | GPL (Tudarco)

Leave a Comment