
Raia 173 wa Tanzania waliokuwa wakiishi katika mkoa wa KwaZulu-Natal, Afrika Kusini, wamewasili nchini leo, Agosti 27, 2026, baada ya Serikali kuwawezesha kurejea kwa hiari.
Kundi hilo limesafirishwa kwa ndege maalumu kupitia ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.
Zoezi hilo liliratibiwa baada ya Serikali, kupitia Ubalozi wa Tanzania mjini Pretoria, kutoa wito kwa Watanzania waliokuwa tayari kurejea nyumbani kujisajili na kukamilisha taratibu za safari.
Mpango huo unatarajiwa kutekelezwa kwa awamu katika maeneo mbalimbali ya Afrika Kusini, kwa lengo la kuwawezesha Watanzania wanaohitaji kurejea nchini kufanya hivyo kwa usalama na utaratibu.
Miongoni mwa walionufaika na zoezi hilo ni Watanzania wasio na pasipoti, waliopoteza pasipoti zao au ambao muda wa matumizi ya pasipoti zao umeisha, pamoja na watoto waliozaliwa nchini Afrika Kusini.
Kwa wale wasio na pasipoti, Serikali imewawezesha kupata hati za dharura za kusafiria ili kuwawezesha kurejea nchini.
Hatua hiyo imekuja wakati kukiwa na ongezeko la hisia na maandamano dhidi ya wahamiaji nchini Afrika Kusini, hali ambayo imesababisha baadhi ya mataifa ya Afrika kuchukua hatua za kuwawezesha raia wao kurejea nyumbani.
Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa zoezi hilo ni la hiari na linalenga kuwawezesha wananchi kurejea nchini kwa usalama na kwa kufuata taratibu.
Kurejea kwa raia hao ni sehemu ya juhudi za Serikali, kupitia uwakilishi wake wa kidiplomasia nchini Afrika Kusini, kuwasaidia Watanzania wanaohitaji kurejea nyumbani.
Ubalozi wa Tanzania mjini Pretoria pia hutoa huduma za dharura, masuala ya pasipoti na huduma nyingine za kibalozi kwa raia wa Tanzania nchini Afrika Kusini.
Na Ilankize Godfrey