
Tanga. Airtel Tanzania imepanga kuanzisha kituo cha Airtel Fursa Lab katika Shule ya Sekondari Magaoni, mkoani Tanga, ikiwa ni hatua inayolenga kuwaongezea vijana fursa za kujifunza teknolojia, ubunifu na ujasiriamali.
Kituo hicho kitakuwa na mfumo wa darasa janja (Smart Class) na kinatarajiwa kuwapa wanafunzi na vijana mazingira ya kujifunza, kufanya majaribio na kuendeleza mawazo ya kibunifu yanayoweza kusaidia kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.
Akizungumza wakati wa Wiki ya Taifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu iliyofanyika Tanga, Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando, amesema kituo hicho ni sehemu ya jitihada za kampuni hiyo kuwawezesha vijana kutumia teknolojia kwa tija.
“Kituo hiki kipya kitatoa mazingira ambayo vijana na wabunifu wataweza kujifunza, kufanya majaribio na kuendeleza mawazo yao,” amesema Mmbando.
Amesema kupitia Fursa Lab, vijana wataweza kupata mafunzo katika teknolojia, ujasiriamali na maeneo mbalimbali ya ujuzi wa kidijitali, huku wakipewa nafasi ya kugeuza mawazo yao kuwa miradi yenye suluhisho kwa jamii.
Fursa Lab kuwajengea vijana uwezo
Mpango wa Airtel Fursa Lab ulianzishwa mwaka 2020 kupitia ushirikiano kati ya Airtel Africa Foundation na Dar es Salaam Technology and Business Incubator (DTBi).
Tangu kuanzishwa kwake, zaidi ya watu 5,800, wakiwemo wanafunzi, walimu, vijana, wajasiriamali na wanawake, wamenufaika na mafunzo kupitia mpango huo.
Lengo la Fursa Lab ni kusaidia kuziba pengo kati ya upatikanaji wa teknolojia na uwezo wa kuitumia kwa ajili ya elimu, biashara na ubunifu.
Wanafunzi watumia teknolojia kutatua changamoto
Uzoefu kutoka Airtel Fursa Lab iliyopo Shule ya Sekondari Kijitonyama, Dar es Salaam, unaonyesha namna wanafunzi wanavyoweza kutumia teknolojia kubuni suluhisho kwa changamoto zinazowazunguka.
Miongoni mwa miradi iliyobuniwa ni programu inayomsaidia msichana kufuatilia mzunguko wa hedhi na kupata taarifa muhimu kuhusu afya yake.
Mwanafunzi Angel Swai naye amewahi kubuni wazo linalotumia akili mnemba katika udhibiti wa taa za barabarani, baada ya kutumia vifaa na rasilimali zilizopo katika kituo hicho kujaribu na kuendeleza wazo lake.
Miradi hiyo inaonyesha msisitizo wa Fursa Lab katika kuwasaidia vijana kwenda zaidi ya kujifunza nadharia na kuwapa nafasi ya kutumia teknolojia katika kutengeneza suluhisho halisi.
Ubunifu kuunganishwa na biashara
Kituo kinachotarajiwa kuanzishwa Magaoni pia kitasaidia kuwaunganisha vijana na fursa za biashara kupitia programu zinazolenga kukuza ujasiriamali na ubunifu.
Programu hizo zinaendeshwa kwa ushirikiano wa Airtel Tanzania, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia DTBi, pamoja na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
Kupitia mafunzo hayo, wabunifu watapata uelewa kuhusu haki miliki na namna ya kulinda mawazo yao, huku mafunzo ya ujasiriamali yakilenga kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia kuanzisha na kukuza biashara.
Mmbando amesema Airtel inalenga kuwawezesha vijana na wajasiriamali kutumia vituo hivyo kujenga ujuzi na kubadilisha mawazo yao kuwa bidhaa na huduma zenye thamani kiuchumi.
Mbali na kituo cha Magaoni, Airtel pia inapanga kuanzisha kituo kingine cha Fursa Lab katika eneo la Usagara, Tanga, hatua inayotarajiwa kuongeza zaidi fursa za kujifunza kidijitali na ubunifu kwa vijana wa mkoani humo.
Hatua hiyo inaendelea kuonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi, taasisi za Serikali na wadau wa teknolojia katika kuwaandaa vijana kwa fursa zinazotokana na uchumi wa kidijitali.