×

Vodacom Yaja na Ubunifu Mpya Kuelekea Tanzania 2050

Katika toleo la 12 la Wiki ya Ubunifu Tanzania (IWTz) 2026, Vodacom Tanzania imezidi kuonyesha jinsi mtandao, ubunifu na ujasiriamali vinavyochangia malengo ya Dira ya Maendeleo Tanzania 2050.

Tukio hili linakutanisha wabunifu wajasiriamali, watunga sera, watafiti, wawekezaji, vijana, wadau wa maendeleo na viongozi wa sekta binafsi chini ya kauli mbiu: “Kutoka Matarajio hadi Mageuzi: Kuibua Njia ya Tanzania Kuelekea Ustawi Jumuishi.”

Katika wiki hii, Vodacom imeshiriki katika mijadala mbalimbali kuhusu uchumi wa wabunifu wa maudhui, banda la maonyesho, mijadala na wanahabari na wadau, uzinduzi wa Vodacom Accelerator Season 5, pamoja na onyesho la moja kwa moja la usalama wa mtandao (cybersecurity) litakalofuatiwa na jopo la majadiliano.

Akizungumza katika majadiliano ya kuziunganisha Sauti za Watanzania: Watengeneza maudhui na Majukwaa Mtandaoni. Mkuu wa Idara ya Chapa na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Yvonne Maruma, alisema thamani ya mtandao inapaswa kupimwa kwa kile unachowawezesha watu kufanya.

“Mtandao ni hatua ya kwanza ya kushiriki katika uchumi wa kidijitali. Lakini thamani yake halisi iko katika kile unachowawezesha watu kufanya: kujifunza, kubuni, kujenga biashara, kufikia hadhira na kusikika,” alisema Maruma.

“Kwa kijana wa Kitanzania, simu janja inaweza kuwa darasa, soko, studio ya ubunifu na chombo cha biashara. Wakati Tanzania ikitekeleza Dira 2050, wabunifu wa maudhui wanapaswa kuonekana zaidi ya njia za kusambaza ujumbe; wao ni washirika wanaoweza kugeuza mawazo ya ujasiriamali, elimu, ujumuishaji wa kifedha na ubunifu kuwa hadithi ambazo watu wanaelewa, wanaziamini na kuzifanyia kazi. Hilo ndilo tunalomaanisha tunaposema Vodacom ni Zaidi ya Mtandao.”

Kupitia mpango wa Vodacom Youth Base (VYB), kampuni inaendelea kushirikiana na watengeneza maudhui mtandaoni na kuwasaidia kubaki mtandaoni wakati wakitengeneza na kusambaza maudhui kwa hadhira zao.

Mpango huu ni sehemu ya jitihada pana za Vodacom za kuhakikisha ujumuishaji wa kidijitali wenye maana, unaowawezesha watu si tu kuunganishwa mtandaoni, bali pia kushiriki, kushindana na kuongoza katika uchumi wa kidijitali.

Katika kilele cha wiki hii, Vodacom Tanzania itazindua programu ya Vodacom accelerator season 5, ambayo imelenga kuwasaidia wajasariamali wa Kitanzania kuanzia hatua zao za mwanzo za wazo hadi kuwa biashara imara. Uzinduzi huu utaambatana na hadithi ya mmoja wa wahitimu wa awali wa mpango huu aliyefanikiwa kutoka wazo hadi biashara.

Ushiriki wa Vodacom katika Wiki ya Ubunifu Tanzania unajengwa juu ya ushirikiano wake na UNDP Tanzania na unaunga mkono malengo ya Dira ya Maendeleo Tanzania 2050: uchumi wa viwanda wenye ushindani wa dola trilioni 1 za Marekani, unaoendeshwa na mtandao jumuishi wa usafirishaji, nishati, sayansi na teknolojia, utafiti na maendeleo, pamoja na mageuzi ya kidijitali.

Leave a Comment