×

Kesi ya Uhaini ya Lissu Yaendelea, Mnyika Aeleza Mahakama Msimamo wa Chadema

Usikilizwaji wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, unaendelea leo Septemba 2, 2026, ikiwa ni hatua ya kuendelea na maswali ya dodoso kwa shahidi wa pili wa upande wa utetezi, John Mnyika, ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho.

Hapo jana, Septemba 1, 2026, katika mwendelezo wa maswali ya upande wa Jamhuri kwa shahidi huyo, Mnyika alihojiwa kuhusu msimamo wa kisiasa wa CHADEMA kuhusu kauli ya “No Reforms, No Election”, pamoja na vitendo vya vurugu vilivyotokea mwaka uliopita.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, amekabiliwa na maswali mazito kuhusu suala la fedha zinazohusishwa na mpango unaotajwa kama “Tone Tone”, katika mahojiano ya kina yaliyofanyika mahakamani.

Mnyika amesisitiza kuwa chama hicho hakikubagua mtu katika suala hilo, akisema: “Mikono yetu ni safi. Sisi hatuna ubaguzi.”

Katika mahojiano hayo, wakili Job alimuuliza Mnyika iwapo malipo ya fedha za “Tone Tone” kwa watu wachache, iwapo yalifanyika kwa ubaguzi, yangekuwa ukiukwaji wa Katiba.

Mnyika alijibu kwa kusisitiza kuwa kuna vipaumbele vilivyo wazi, huku akipinga hoja kwamba Chadema imehusika katika ubaguzi.

Wakili Job pia alimuuliza Mnyika kuhusu msimamo wake kwamba si kila mzozo unapaswa kutatuliwa mahakamani. Mnyika alisema chama kimekuwa kikijaribu kushauriana na kutafuta suluhu katika kila hatua kabla ya kufikia hatua nyingine.

Sehemu nyingine ya maswali ilihusu Ishengoma Mtembey Barongo, ambaye Job alimtaja kuwa Katibu wa Kata ya Mikocheni na mwanachama wa Chadema.

Mnyika alisema hamfahamu mtu huyo, na alipoulizwa kuhusu video iliyosambaa mitandaoni inayodaiwa kumuonyesha akieleza mipango ya kuvuruga uchaguzi, Mnyika alisema hawezi kutoa maoni kwa kuwa hajawahi kuiona video hiyo.

“Siwezi kusema kwa sababu sijaona hiyo clip,” alisema Mnyika.

Akifafanua mfumo wa uongozi wa Chadema, Mnyika alisema makatibu wa kata wanasimamia shughuli za chama katika ngazi hiyo na wanaripoti kwa ngazi ya jimbo, hivyo Katibu Mkuu hahusiki moja kwa moja na shughuli zao za kila siku.

Alisema pia maelekezo kutoka ngazi ya taifa hupitia mfumo wa uongozi kutoka kanda, mikoa, wilaya, majimbo na hatimaye kata.

Katika sehemu nyingine ya ushahidi wake, Mnyika alikataa kukubaliana na hoja kwamba mahakama ndiyo njia bora ya kutatua kila jambo ambalo mtu hakubaliani nalo.

Alikiri kuwa mahakama ina mamlaka ya kusikiliza mashauri ya kikatiba, lakini alipoulizwa kama njia bora ya kupata suluhu inapokuwa na kutoridhishwa ni kwenda mahakamani, alijibu:

Mnyika alisema Chadema imekuwa ikitumia njia za mazungumzo na mashauriano katika kushughulikia changamoto mbalimbali.

Mahojiano hayo yameendelea kuibua maswali kuhusu uendeshaji wa chama, mfumo wa mawasiliano kutoka uongozi wa taifa hadi ngazi za chini, pamoja na tuhuma na madai yanayohusishwa na suala la “Tone Tone”.

Mwisho wa dodoso hilo, upande wa mahojiano ulitangaza kuwa umefikia mwisho wa kumuuliza Mnyika maswali.

Job: Je, Tundu Antipas Lissu amewahi kufungua kesi ya kikatiba kwa jina lake binafsi?

Mnyika: Kwa mujibu wa ufahamu wangu, sifahamu.

Job: Utakubaliana na mimi sasa, shahidi, kwamba kwa mujibu wa sheria mahakama imepewa mamlaka ya kusikiliza mashauri ya kikatiba?

Mnyika: Ni kweli.

Job: Utakubaliana na mimi kwamba njia bora ya kupata utatuzi, usiporidhishwa na jambo, ni kwenda mahakamani?

Mnyika: Sikubaliani na wewe.

Job: Mshitakiwa kabla ya kutoa ushahidi alisema anataka kukuandaa. Alikuambia nini?

Mnyika: Aliniambia taratibu za kufuata tu ninapokuwa kizimbani.

Job: Nitamuomba shahidi. Waheshimiwa Majaji, ukiwa kama Katibu Mkuu, unamfahamu Ishengoma Mtembey Barongo?

Mnyika: Sijui.

Job: Je, unafahamu huyu ni Katibu wa Mikocheni?

Mnyika: Simfahamu.

Job: Je, unafahamu huyu bwana Ishengoma ni mwanachama wa Chadema?

Mnyika: Hayo yatakuwa ni maoni yako.

Job: Hawa makatibu wa kata, utaratibu wa kufanya kazi ukoje?

Mnyika: Wao ndio wasimamizi wa shughuli za chama kwenye kata na wanaripoti kwenye jimbo, hivyo Katibu Mkuu hahusiki moja kwa moja.

Job: Ikitokea kuna ushahidi kuwa huyu ni mwanachama wa Chadema na mnamkana?

Mnyika: Ngazi ya kata inahudumiwa na jimbo. Muite Katibu wa Jimbo umuulize swali hilo.

Job: Hebu wajibu Waheshimiwa Majaji, maelekezo yakitoka ngazi ya taifa yanafikaje kwenye ngazi ya kata?

Mnyika: Chama taifa kinawasiliana na makatibu wa kanda. Wao wanashusha kwenye mikoa, mikoa inashusha kwenye wilaya, kisha majimbo na kata.

Job: Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, kinaamini katika matumizi ya TEHAMA katika kuhabarisha umma?

Mnyika: (Anasoma katiba) kuhakikisha chama kinatumia TEHAMA kukiunga mkono, hivyo jibu ni sahihi.

Job: Unakubaliana na mimi kwamba kitendo cha fedha za Tone Tone kulipa kwa watu wachache ni ukiukwaji wa katiba?

Mnyika: Kuna kipaumbele ambacho kipo wazi.

Job: Kama hizo fedha chache zimelipwa kwa ubaguzi, unaona wapi uhalali wa kuzungumzia uhuru na haki?

Mnyika: Mikono yetu ni safi. Sisi hatuna ubaguzi. Nyie serikali ndio mna ubaguzi kwa kuzuia ruzuku yetu.

Job: Usipoaminika kwa dogo, huwezi kuaminika kwa kubwa.

Mnyika: Tunaaminika kwa dogo na makubwa.

Job: Una uzoefu wako wa kutunga sheria. Unaona hatukushauriwa vyema kwa kutofuata njia ya mahakama?

Mnyika: Hapana. Tumejaribu kushauriana vyema kila hatua.

Job: Ulisema humfahamu Ishengoma Mutembei Barongo. Huyo bwana Mutembei ndiye Katibu wa Kata wa Mikocheni.

Mnyika: Siwezi kukubaliana na mambo nisiyoyafahamu.

Job: Utakubaliana kwamba video clip iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, bwana Mutembei alieleza mipango ya kuvuruga uchaguzi ilitoka juu ndani ya chama?

Mnyika: Siwezi kusema kwa sababu sijaona hiyo clip.

Job: Ni hayo tu, Waheshimiwa Majaji.

Nzengelei: Waheshimiwa Majaji, tumefikia mwisho wa kumuuliza maswali ya dodoso shahidi huyu.

Tundu Lissu anashtakiwa kwa kosa la uhaini chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania, kama ilivyorekebishwa mwaka 2023.

Shtaka hilo linatokana na madai ya upande wa Jamhuri kwamba, mnamo Aprili 3, 2025, Lissu alitoa maneno na maandishi yaliyolenga kuhamasisha umma na kushinikiza viongozi wakuu wa Serikali ili kuzuia au kuvuruga mchakato wa uchaguzi.

Usikilizwaji wa kesi hiyo unaendelea Mahakamani, huku upande wa utetezi ukiendelea na ushahidi wake kupitia shahidi John Mnyika.

Leave a Comment