
Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu, amewataka watendaji wa Serikali, hususan wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kubadili haraka mtazamo wao na kuacha kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).
Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo, Alhamisi, Septemba 3, 2026, Zungu amesema hivi karibuni Rais alitoa maelekezo na kukemea hali ya uchafu katika Jiji la Dar es Salaam, lakini changamoto kubwa imekuwa kwa watendaji wa TAMISEMI ambao, kwa mujibu wake, wamekuwa kikwazo katika kutafuta suluhisho la tatizo hilo.
Amesema halmashauri za Dar es Salaam na miji mingine mikubwa nchini zinapobuni miradi ya PPP kwa ajili ya kuboresha usafi wa miji na kuiwasilisha TAMISEMI kwa ajili ya kushughulikiwa, majibu kutoka ofisi hiyo yamekuwa yakichelewa au kutotolewa kabisa.
Zungu amesema hali hiyo imekuwa ikiwakatisha tamaa wawekezaji wanaohitaji kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi ya usafi, na matokeo yake miji hiyo imeendelea kukabiliwa na changamoto ya uchafu.
Ametoa wito kwa watendaji hao kubadili fikra na kuhakikisha miradi ya PPP inayowasilishwa inashughulikiwa kwa wakati ili kutoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika kutatua changamoto zinazozikabili halmashauri.