×

Gamondi Atangaza Kikosi Cha Taifa Stars Kwa Ajili ya AFCON 2027

Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Miguel Ángel Gamondi, ametangaza kikosi cha awali kitakachoingia kambini hivi karibuni kwa ajili ya kujiandaa na michezo mbalimbali ya kimataifa.

Kikosi hicho kimeandaliwa kwa ajili ya michezo miwili muhimu ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 dhidi ya Guinea-Bissau na Madagascar, pamoja na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Ghana.

Tangazo la kikosi hicho limetolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii, huku likiwavutia na kuwapa matumaini mashabiki wa soka nchini.

Kikosi hicho kinaonekana kuwa na mabadiliko kadhaa katika majina ya wachezaji walioitwa, hali inayotarajiwa kutoa ushindani mkubwa wakati Taifa Stars itakapoanza maandalizi yake kuelekea michezo hiyo.

Gamondi anatarajiwa kutumia kambi hiyo kuwafanyia tathmini wachezaji walioitwa, kuimarisha mfumo wa timu na kuweka mikakati itakayoiwezesha Taifa Stars kupata matokeo mazuri katika michezo yake ya kufuzu AFCON 2027.

Michezo dhidi ya Guinea-Bissau na Madagascar itakuwa sehemu muhimu ya safari ya Tanzania kuelekea fainali hizo, huku mchezo dhidi ya Ghana ukitoa nafasi kwa benchi la ufundi kuwapima wachezaji na kufanya maandalizi zaidi kabla ya michezo ya ushindani.

Mashabiki wa Taifa Stars sasa wanaelekeza macho yao kwenye kambi hiyo, wakisubiri kuona sura mpya na namna Gamondi atakavyokisuka kikosi hicho katika harakati za Tanzania kutafuta nafasi ya kushiriki AFCON 2027.

Na Peter Jinanai | GPL

 

Leave a Comment