×

Netanyahu Atishia Kuipindua Serikali ya Iran ‘Utawala Wao Upo Dhaifu’

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema kuuangusha utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kunawezekana, akidai kuwa serikali hiyo kwa sasa ni dhaifu kuliko wakati mwingine wowote na inapambana kusalia madarakani.

Netanyahu amesema hayo Alhamisi, Septemba 3, 2026, wakati akizungumza katika hafla ya Mwaka Mpya wa Kiyahudi, Rosh Hashanah, iliyowakutanisha viongozi waandamizi wa kijeshi wa Israel.

Amesema ana imani kuwa Israel inaweza kuondoa kabisa tishio linalotokana na Iran, akisisitiza kuwa kuuangusha utawala wa Tehran ni miongoni mwa majukumu makuu yaliyosalia mbele ya Israel na kwamba lengo hilo sasa liko ndani ya uwezo wao.


Netanyahu pia amesema Iran kutolenga Israel katika awamu ya hivi karibuni ya mashambulizi si jambo la bahati mbaya, akidai kuwa Tehran inafahamu nguvu za kijeshi, silaha na azma ya Israel.

Kauli hizo zimekuja wakati mvutano kati ya Israel na Iran ukiendelea kuwa mkubwa, huku Iran ikiendelea kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo yanayohusishwa na Marekani katika Mashariki ya Kati.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, ameonya kuwa endapo Iran itashambulia Israel wakati wa sikukuu za Kiyahudi, nchi hiyo itajibu kwa nguvu kubwa, ikilenga miundombinu ya kijeshi na ya kiraia ya Iran.

Wakati huohuo, uchaguzi wa bunge la Israel umepangwa kufanyika Oktoba 27, 2026, huku Netanyahu akitarajiwa kuendelea kuwa mhusika mkuu katika mchakato huo wa kisiasa.

Leave a Comment