
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amezitaka Mamlaka na Taasisi zinazohusika kuchukua hatua za haraka za maandalizi ili kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza mwezi Oktoba 2026.
Makamu wa Rais ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa ya utayari na maandalizi ya Serikali kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kuhusu uwezekano wa mvua hizo.
Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi ya Makamu wa Rais jijini Dar es Salaam, kikihudhuriwa na viongozi na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wizara ya Ujenzi pamoja na taasisi zilizo chini ya wizara hizo.

Katika kikao hicho, Ndejembi amesisitiza umuhimu wa taasisi zote zinazohusika kufanya kazi kwa pamoja na kuchukua hatua za tahadhari mapema ili kuzuia au kupunguza athari zinazoweza kuwakumba wananchi.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuvishirikisha Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika maandalizi hayo ili kuhakikisha kunakuwa na nguvu kazi ya kutosha na kuimarisha uwezo wa Serikali wa kukabiliana kwa haraka na madhara yatakayoweza kujitokeza.
“Ifanyike kampeni ya haraka, mikondo na mifereji ya maji izibuliwe, na barabara ziandaliwe,” amesisitiza Makamu wa Rais.
Aidha, Ndejembi ameelekeza taka, tope na udongo unaotolewa wakati wa kuzibua mitaro na mifereji kuondolewa mara moja na kutupwa katika maeneo yaliyotengwa, badala ya kuachwa kandokando ya barabara ambako vinaweza kurejea kwenye mifereji wakati mvua zitakapoanza.
Makamu wa Rais pia amezitaka mamlaka husika kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa barabara ili kuhakikisha vifusi vilivyorundikwa katika maeneo ya ujenzi vinasambazwa kwa wakati.
Amesisitiza kuwa hatua hizo zinapaswa kuchukuliwa mapema kabla ya mvua kuanza, kwani kusubiri hadi mvua zinyeshe kunaweza kuongeza usumbufu na kero kwa wananchi.