Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanzilishi pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF), Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amewasili mkoani Tabora leo Jumamosi, Septemba 12, 2026, kwa ziara ya siku nne.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kikwete atatembelea na kukagua zahanati zilizojengwa na JMKF kwa lengo la kusaidia juhudi za Serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa maeneo ya pembezoni.

Zahanati hizo zimejengwa kwa lengo la kuwahudumia zaidi ya wakazi 36,000 katika vijiji viwili pamoja na jamii zinazozunguka maeneo hayo.
Mbali na kukagua miundombinu hiyo ya afya, Dkt. Kikwete anatarajiwa pia kuangalia utekelezaji wa Mradi wa Jamii Salama (Mobile Antenatal Care Outreach), unaolenga kusogeza huduma za afya kwa wajawazito karibu na jamii.

Dkt. Kikwete amepokelewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Upendo Wella, pamoja na viongozi mbalimbali wa mkoa huo.
Ziara hiyo inatarajiwa kutoa fursa ya kutathmini maendeleo ya miradi hiyo, pamoja na namna inavyosaidia kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu za afya kwa wananchi wa maeneo yanayozunguka vijiji hivyo.
