×

Stanbic Yatoa Milioni 100 Kuunga Mkono Nyerere Cycling Tour 2026

Benki ya Stanbic Tanzania imetoa shilingi milioni 100 kuunga mkono Nyerere Cycling Tour 2026, msafara wa baiskeli unaolenga kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa vitendo.

Safari hiyo inaanza Dar es Salaam Oktoba 4, 2026, kwa mbio za baiskeli kuelekea Bagamoyo, kabla ya msafara rasmi wa kuelekea Butiama kuanza Oktoba 5. Zaidi ya waendesha baiskeli 200 kutoka ndani na nje ya Tanzania wanatarajiwa kushiriki safari hiyo yenye urefu wa kilomita 1,415, ambayo itahitimishwa Butiama, Mara, Oktoba 14.

Katika kuendeleza falsafa ya Mwalimu Nyerere ya kupambana na ujinga, maradhi na umaskini, Stanbic imeungana na waandaaji kuwezesha miradi ya kijamii katika mikoa yote 10 itakayopitiwa na msafara huo.

Kwa mwaka huu, zaidi ya Watanzania 25,000 wanatarajiwa kunufaika na miradi hiyo, ikiwemo ujenzi wa madarasa 10, ukarabati wa madarasa 40, utoaji wa madawati 1,000 na upandaji wa miti 1,100.

Aidha, wataalamu wa Stanbic Bank wenye ithibati kutoka Benki Kuu ya Tanzania watatoa elimu ya fedha bila malipo katika maeneo yote yatakayopitiwa na msafara.

Ushirikiano huo ni sehemu ya makubaliano ya miaka mitatu kati ya Stanbic, Vodacom na waandaaji wa Nyerere Cycling Tour kuanzia 2025 hadi 2027, yenye thamani ya shilingi milioni 300, ambapo Stanbic inachangia shilingi milioni 100 kila mwaka.

Leave a Comment