×

Watuhumiwa 37 Wahukumiwa Kwa Makosa Mbalimbali Ya Jinai Kilimanjaro

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linaendelea kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa wananchi pamoja na mali zao, huku likiendelea kuchukua hatua dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa sheria.

Katika kipindi cha mwezi Agosti 2026, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro lilifanya operesheni mbalimbali za kukabiliana na makosa ya jinai na makosa mengine yanayohatarisha usalama na ustawi wa jamii.

Operesheni hizo zimewezesha kukamatwa kwa jumla ya watuhumiwa 242 wa makosa mbalimbali ya jinai, ambapo baadhi ya kesi zao zimefikishwa Mahakamani baada ya kukamilika kwa taratibu za uchunguzi na upelelezi.

Jumla ya watuhumiwa 69 walikamatwa kwa makosa ya maadili dhidi ya jamii.

– Watuhumiwa 17 walikamatwa kwa kosa la kupatikana na dawa za kulevya aina ya bhangi, ambapo jumla ya gramu 722 zilikamatwa na kesi 22 zilifunguliwa.

– Watuhumiwa 28 walikamatwa kwa kosa la kupatikana na/kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi, ambapo jumla ya kilo 95.2 zilikamatwa na kesi 46 zilifunguliwa.

– Watuhumiwa 23 walikamatwa kwa kosa la kupatikana na pombe haramu aina ya gongo, ambapo jumla ya lita 420.5 zilikamatwa na kesi 36 zilifunguliwa.

– Mtuhumiwa mmoja alikamatwa baada ya kupatikana na mitambo miwili ya kutengenezea pombe haramu aina ya gongo, ambapo kesi moja ilifunguliwa.

– Watuhumiwa wawili walikamatwa wakiwa na nyara za Serikali, ambapo jumla ya kilo 16 za nyama ya wanyamapori aina ya swala na nyumbu zilikamatwa na kesi tatu zilifunguliwa.

Kwa upande wa uhamiaji haramu, kesi mbili zilifunguliwa dhidi ya raia wa nchi jirani waliokutwa wameingia nchini bila kibali.

Katika makosa yanayohusiana na mazao ya misitu, kesi 10 zilifunguliwa na watuhumiwa wanane walikamatwa wakiwa na jumla ya magogo 13.

WATUHUMIWA 37 WAHUKUMIWA MAHAKAMANI
Kwa upande wa kesi zilizofikishwa Mahakamani ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro, jumla ya kesi 37 zilisikilizwa na mashauri yake kukamilika, ambapo Mahakama zilitoa hukumu mbalimbali dhidi ya watuhumiwa waliopatikana na hatia, ikiwemo hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa makosa dhidi ya binadamu.

 

Leave a Comment