×

Kikwete Atoa Ujumbe Mzito kwa Wanaume Kuhusu Saratani ya Tezi Dume

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amewataka wanaume kujenga utamaduni wa kupima afya ya tezi dume mara kwa mara, akisema uchunguzi wa mapema huongeza uwezekano wa kupata matibabu kwa wakati kabla saratani haijasambaa.

Dkt. Kikwete ametoa wito huo jijini Dar es Salaam alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Mwezi wa Uelewa wa Saratani ya Tezi Dume yaliyofanyika katika Hospitali ya Kairuki, Mikocheni.

Katika maadhimisho hayo, Dkt. Kikwete alitembelea mtambo wa kisasa wa High Intensity Focused Ultrasound (HIFU), unaotumika kutibu baadhi ya uvimbe, ikiwamo saratani ya tezi dume kwa wagonjwa wanaostahili, bila kufanyiwa upasuaji wa kawaida. Teknolojia hiyo hutumia mawimbi ya sauti yenye nguvu kuelekeza joto katika eneo lenye uvimbe.

Akizungumza kuhusu uzoefu wake binafsi, Dkt. Kikwete alisema alipogundulika mapema kuwa na dalili za saratani ya tezi dume mwaka 2014, aliamua kufanyiwa uchunguzi wa kina nchini Marekani. Vipimo vilichukuliwa na kuthibitisha kuwa saratani ilikuwa katika hatua za awali, hali iliyomwezesha kuchukua hatua za matibabu mapema.

“Walichukua sampuli 14 na katika sampuli mbili wakaona dalili za saratani. Madaktari wakaniambia kuwa ilikuwa inaanza na kwamba ingeweza kutibika,” alisema.

Alisema alikubali kufanyiwa upasuaji wa kuondoa tezi dume ili kuzuia saratani hiyo isisambae katika sehemu nyingine za mwili, na kwamba tangu wakati huo ameendelea kuwa na afya njema.

“Baada ya kufanyiwa upasuaji nilijenga utaratibu wa kupima afya yangu mara kwa mara. Kwa sasa afya yangu ni njema kabisa; ndiyo maana mtu akisema ninaumwa, nacheka tu, kwa sababu ninaifahamu afya yangu,” alisema.

Leave a Comment