×

CCM Yapongeza ACT-Wazalendo Kuwasilisha Jina la Makamu wa Kwanza

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimepongeza uteuzi wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kikisema hatua hiyo imekamilisha muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kisiwandui, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Zanzibar, Khamis Mbeto Hamisi, amesema CCM imempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kutekeleza matakwa ya Katiba.

Mbeto pia amepongeza Chama cha ACT-Wazalendo kwa kuwasilisha jina la mgombea kwa nafasi hiyo, akisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa misingi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Amesema kwa mujibu wa Ibara ya 39 ya Katiba ya Zanzibar, Serikali hiyo inatakiwa kuwa na Makamu wa Kwanza na Makamu wa Pili wa Rais, pamoja na majukumu yao yaliyoainishwa kikatiba.

Kwa mujibu wa Mbeto, ACT-Wazalendo sasa inapaswa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kuzingatia Katiba na sheria za Zanzibar.

Amesema CCM inatarajia viongozi watakaounda Serikali hiyo, wakiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais na mawaziri, kufanya kazi kwa kuzingatia maslahi ya wananchi, Dira ya Taifa ya 2050 pamoja na mipango ya maendeleo ya Zanzibar.

Mbeto amesisitiza umuhimu wa viongozi wa kisiasa kutumia kauli zinazojenga umoja na mshikamano, huku akivitaka vyama vya siasa na wafuasi wao kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii ili kuepuka kauli zinazoweza kuleta mgawanyiko.

Amesema licha ya vyama kuendelea na shughuli zao za kisiasa, wanapaswa kutambua kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inalenga kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar.

CCM imesema iko tayari kushirikiana na viongozi wote wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wakiwemo Rais, Makamu wa Kwanza wa Rais, Makamu wa Pili wa Rais, mawaziri na watendaji wengine, katika kuhakikisha serikali inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Mbeto amesema ushirikiano huo unalenga kuimarisha umoja, mshikamano na maendeleo ya Zanzibar, huku akiwataka viongozi na wananchi kutumia fursa hiyo kujenga mazingira yatakayowezesha Zanzibar kupata maendeleo zaidi.

Leave a Comment