×

Video: Kutoka SGR Hadi Wizara ya Ujenzi, Masanja Kadogosa Ateuliwa Waziri

Masanja Kungu Kadogosa ni Mbunge wa Jimbo la Bariadi Vijijini mkoani Simiyu, kupitia chama cha Chama cha Mapinduzi (CCM) ameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Waziri wa Ujenzi, akichukua nafasi iliyoachwa na Abdallah Hamis Ulega, ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Uteuzi huo umetangazwa Jumapili, Septemba 27, 2026, kupitia taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka.

Kadogosa anaingia katika nafasi hiyo akiwa na uzoefu wa muda mrefu katika sekta ya miundombinu, hususan kwenye masuala ya reli na usafiri. Kabla ya kuingia katika siasa, aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika sekta ya fedha na reli.

Kwa miaka kadhaa, Kadogosa alihudumu katika uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), kipindi ambacho Tanzania ilikuwa ikitekeleza mradi mkubwa wa Reli ya Kisasa (SGR).

Safari yake ya kikazi ilianza katika sekta ya benki, ambako aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Mikopo katika Benki ya Maendeleo ya TIB. Mwaka 2016 aliteuliwa kuongoza kampuni ya Reli Tanzania (TRL).

Kadogosa ana shahada ya uzamili ya Utawala wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Umeå nchini Sweden, huku akiwa na uzoefu katika maeneo ya uhasibu, usimamizi wa fedha na benki.

Aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa (katikati) na Profesa John Kondoro (kulia) wakati alipokagua ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR) katika eneo la Mkonze jijini Dodoma, Novemba 24, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Kisiasa, mwaka 2025 aliingia kwenye mchakato wa mchujo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuwania nafasi ya ubunge, kabla ya sasa kuingia katika Serikali kama Waziri wa Ujenzi.

Akiwa Waziri wa Ujenzi, Kadogosa atakuwa na jukumu la kusimamia sekta inayohusisha ujenzi na maendeleo ya barabara, madaraja pamoja na miradi mbalimbali mikubwa ya miundombinu nchini.

Uteuzi wake unakuja wakati ambapo miradi ya miundombinu ikiendelea kuwa sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo ya Tanzania, hivyo utekelezaji na usimamizi wa miradi hiyo utakuwa miongoni mwa maeneo yatakayokuwa chini ya wizara hiyo.

Uapisho wa mawaziri walioteuliwa utafanyika katika tarehe itakayotangazwa baadaye.

Stori na  Mathna Simba | GPL -TUDACO

Leave a Comment