
Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo, ameendelea na kampeni ya kupandisha bendera za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mabalozi wa chama katika jimbo hilo.
Kampeni hiyo imefanyika katika Kata ya Maisome, ambapo bendera za CCM zimepandishwa kwa mabalozi wa chama.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Shigongo amewataka Watanzania kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi, akisema serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
Amewataka pia wanachama wa CCM kuendelea kueleza na kuwasemea wananchi mambo mazuri yanayofanywa na serikali.
Shigongo amesema kampeni ya kupandisha bendera inalenga kufanyika katika jimbo zima la Buchosa, ambapo kila balozi wa CCM atapatiwa bendera ya chama.
Katika ziara hiyo ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM, Shigongo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Maisome, pamoja na vifaa vilivyotolewa kwa ajili ya kusaidia utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema kukamilika kwa kituo hicho kutakuwa mkombozi kwa wakazi wa Kata ya Maisome ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kupata huduma za afya.

Mbunge huyo pia amekagua Shule ya Msingi Kagorogoro, iliyopo Kata ya Maisome, na kupongeza ujenzi wake akisema umefanyika kwa kiwango cha kuridhisha.
Shigongo amewataka viongozi wa CCM kwenda kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika maeneo yao ili kuona hatua zilizofikiwa na changamoto zinazohitaji kushughulikiwa.
Aidha, amewataka wakazi wa Kata ya Maisome na Watanzania kwa ujumla kutambua miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali, ikiwemo ujenzi wa barabara, vituo vya afya na shule.
Amesema wananchi wanaobeza maendeleo yanayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita wanapaswa kuonyeshwa miradi hiyo ili waweze kuona hatua zilizofikiwa.
Shigongo amesema serikali imefanya mambo mengi ya maendeleo, hivyo ni wajibu wa wanachama na viongozi kueleza kwa wananchi yale yanayotekelezwa.