×

Ndege ya Jeshi la Anga Nigeria Yadondoka, Watu 32 Walikuwa Ndani

LAGOS, Nigeria — Ndege ya Jeshi la Anga la Nigeria imeanguka leo Jumatatu Oktoba 5, 2026 katika jimbo la Ondo, kusini-magharibi mwa nchi hiyo, ikiwa na watu 32 ndani.

Kwa mujibu wa Jeshi la Anga la Nigeria, ndege hiyo ilikuwa katika safari ya kawaida kutoka Benin City kuelekea Lagos, kabla ya kuanguka eneo la Igbokoda, Ondo.

Waziri wa Usafiri wa Anga wa Nigeria, Festus Keyamo, alisema watu 25 walikuwa abiria huku wengine saba wakiwa wafanyakazi wa ndege.

Mamlaka zilisema mabaki ya ndege hiyo yamepatikana karibu na kituo cha jeshi la wanamaji. Vikosi vya uokoaji pamoja na taasisi nyingine za dharura vinaendelea na operesheni ya utafutaji na uokoaji.

Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha watu wakikusanyika karibu na mto huku waokoaji wakitumia boti katika shughuli za utafutaji.

Hadi sasa, mamlaka hazijatoa taarifa rasmi kuhusu idadi ya waliofariki au kujeruhiwa. Uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali hiyo pia unaendelea.

Leave a Comment