
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amesema kiwango cha riba kwa robo ya nne ya mwaka 2026 kitabaki katika asilimia 6.25, sawa na kiwango kilichowekwa katika robo iliyopita.
Uamuzi huo umefikiwa na Kamati ya Sera ya Fedha, ambayo imeamua kuendelea na kiwango hicho kwa robo ya mwaka inayoishia Desemba 2026.
BoT imesema hatua hiyo inalenga kusaidia kudhibiti mfumuko wa bei na kuwezesha ukuaji endelevu wa uchumi.

Akizungumza kuhusu mwenendo wa uchumi, Tutuba amesema ongezeko la bei za mafuta pamoja na matarajio ya mvua za El Niño vinaweza kuongeza shinikizo la mfumuko wa bei katika kipindi kijacho.
Amesema hatua mbalimbali za kisera, kwa kushirikiana na Serikali, zinaendelea kuchukuliwa ili kudhibiti mfumuko wa bei na kupunguza athari za kuongezeka kwa gharama za huduma mbalimbali.
Aidha, amesema kasi ya ukuaji wa uchumi duniani inatarajiwa kupungua ikilinganishwa na mwaka 2025, kutokana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kuikabili hali ya uchumi wa dunia.
