
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati, ikiwemo Shilingi trilioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umeme mkoani Mbeya.
Amesema uwekezaji huo unalenga kuimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, kuchochea ukuaji wa viwanda na biashara, pamoja na kufungua fursa mpya za uwekezaji zitakazochangia maendeleo ya kiuchumi nchini.

Makamu wa Rais ameyasema hayo leo, Oktoba 16, 2026, wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Kupokea na Kusambaza Umeme cha Iganjo, mkoani Mbeya.
Amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya umeme na kuongeza uwezo wa nchi katika kukidhi mahitaji ya nishati kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji.

Kwa mujibu wa Ndejembi, uwekezaji huo hautawanufaisha wananchi wa Mbeya pekee, bali pia utafungua fursa katika sekta za madini, viwanda na biashara, huku ukiimarisha nafasi ya Tanzania katika ushirikiano wa kiuchumi na nchi jirani.
Ameeleza kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika utaiwezesha Tanzania kuongeza uwezo wa kusambaza umeme katika nchi jirani, hatua inayotarajiwa kuchochea biashara ya nishati na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.

Aidha, amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutaimarisha nafasi ya Jiji la Mbeya kama lango muhimu la biashara na uchumi katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kutokana na umuhimu wake wa kimkakati katika kuunganisha Tanzania na mataifa mengine ya ukanda huo.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameipongeza Wizara ya Nishati pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa usimamizi na utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi.
Amesema ana matumaini kuwa ifikapo Desemba 2026, Kituo cha Kupokea na Kusambaza Umeme cha Iganjo kitakuwa kimewashiwa umeme na kuanza kutoa huduma zitakazowanufaisha wananchi na wadau mbalimbali wa kiuchumi.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi, kuongeza fursa za ajira na kuimarisha uchumi kupitia upatikanaji wa nishati ya uhakika.
