
Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ametangaza kuanza mgomo wa kutokula chakula kuanzia Jumatatu, Oktoba 26, 2026, akipinga kunyimwa haki ya kukutana na mawakili wake kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Mahakama Kuu ya Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Oktoba 24, 2026, Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Rugemeleza Nshala, amesema Lissu amechukua uamuzi huo kwa sababu anataka kutekelezwa kwa uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa wiki iliyopita, unaomtambua kuwa na haki ya kukutana na mawakili wake.
Dkt. Nshala amesema hali hiyo imejitokeza baada ya mawakili wa Lissu, Nashon Nkungu na Paul Kisabo, kwenda Gereza la Ukonga kwa lengo la kukutana na mteja wao, lakini uongozi wa gereza hilo ukawaeleza kuwa mazungumzo hayo yangefanyika kwa utaratibu ambao tayari ulikuwa umekataliwa na Mahakama.

Amesema utaratibu huo ulihusisha Naibu Mkuu wa Gereza, mwanasheria na maafisa wengine kuwepo ndani ya chumba wakati Lissu akizungumza na mawakili wake, jambo ambalo limeelezwa kuwa kinyume na maelekezo ya Mahakama.
Kwa mujibu wa Dkt. Nshala, Lissu alikataa kuzungumza na mawakili wake akidai kuwa amri ya Mahakama inataka maafisa wa gereza wakae umbali unaowawezesha kuwaona, lakini wasiweze kusikia mazungumzo yao.
Dkt. Nshala ameongeza kuwa baadaye alikwenda mwenyewe gerezani kwa lengo la kukutana na Lissu, lakini awali aliambiwa kuwa Lissu hakuwa tayari kuzungumza. Hata hivyo, alisisitiza kutaka kuonana naye na alipofanikiwa kukutana naye, Lissu alieleza msimamo wake kuwa hatazungumza na mawakili wake hadi pale amri ya Mahakama itakapotekelezwa.
Hatua ya Lissu kutangaza mgomo wa kutokula chakula inaibua mjadala kuhusu utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama na haki ya mtuhumiwa kukutana na mawakili wake kwa kufuata masharti yaliyowekwa na Mahakama.