
Jeshi la Polisi Tanzania limetoa onyo kwa watu wanaojihusisha na mipango ya kufanya vurugu, fujo na kuharibu miundombinu inayotumika kutoa huduma kwa umma, mali za umma na binafsi, likisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Katika taarifa iliyotolewa Oktoba 26, 2026, na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu ya Polisi Dodoma, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Alphonce Misime.
Jeshi hilo limesema linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulinda amani, utulivu na usalama nchini.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa, licha ya kuwepo kwa mipango, matamko na uhamasishaji unaofanywa na baadhi ya viongozi wa dini, siasa na wanaharakati wanaoishi ndani na nje ya nchi, kuhusu kuhamasisha watu kujiingiza katika vitendo vya uhalifu, linaendelea kufuatilia kwa karibu mipango hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Aidha, Jeshi hilo limeonya kuwa vitendo vya kihalifu vinavyopangwa ni pamoja na kufanya vurugu na fujo, kuharibu miundombinu inayotumika kutoa huduma kwa umma pamoja na kuharibu mali za umma na binafsi.
Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi kuwa linaendelea kufuatilia kwa karibu taarifa hizo na kuwakamata wahusika watakaobainika kujihusisha na mipango hiyo, ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Vilevile, limewataka watu wanaojihusisha na mipango hiyo kuacha mara moja vitendo hivyo, likisisitiza kuwa sheria itachukua mkondo wake kwa yeyote atakayebainika kuhusika.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kuzingatia sheria za nchi na kutii utawala wa sheria, likieleza kuwa hayo ndiyo mambo muhimu katika kudumisha amani, utulivu na usalama wa Taifa.
