×

Ulega Asisitiza Umuhimu wa Utawala Bora Kama Nguzo Muhimu ya Kudumisha Amani

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, amesisitiza kuwa Utawala Bora unahitaji viongozi na watendaji kusikiliza wananchi, kushughulikia malalamiko yao kwa wakati na kutoa mrejesho kuhusu hatua zilizochukuliwa ili kuimarisha uwajibikaji na imani ya wananchi kwa Serikali.
Waziri Ulega ameyasema hayo leo, Oktoba 26, 2026, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Uraia na Utawala Bora kwa Viongozi na Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa mkoani Manyara.
Amesema viongozi wanapaswa kuweka kumbukumbu sahihi za malalamiko, hatua zinazochukuliwa na mrejesho unaotolewa kwa wananchi ili kuhakikisha kero zao zinafuatiliwa na kutatuliwa kwa ufanisi. Aidha, amewataka viongozi kuwashirikisha wananchi katika mipango ya maendeleo na maamuzi yanayohusu maisha yao.
Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanaakisi falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kufanya kazi kwa kuzingatia utu, akisisitiza kuwa madaraka ni dhamana inayopaswa kutumiwa kwa manufaa ya umma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Martine Shigela, ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kutoa mafunzo hayo, akieleza kuwa yatasaidia kuimarisha utawala bora, uzingatiaji wa sheria na utu katika utendaji wa viongozi na watumishi wa umma.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Shekalaghe, amesema katika miaka miwili ya fedha 2024/2025 na 2025/2026, jumla ya viongozi na watendaji 8,340 walipatiwa mafunzo katika halmashauri 133 zilizopo kwenye mikoa 20.

Leave a Comment