×

Stanbic Yawekeza Kwa Vijana, Safari ya Farid Ally Yatoa Taswira ya Uongozi wa Kesho

Dar es Salaam, Tanzania, Jumatano, Novemba 11, 2026: Vijana viongozi kutoka zaidi ya nchi 190 walipokutana jijini Cape Town, Afrika Kusini, wiki iliyopita kwa ajili ya Mkutano wa Kimataifa wa One Young World, Benki ya Stanbic Tanzania iliwakilishwa na mmoja wa wafanyakazi wake ambaye safari yake ya kikazi inaonesha matokeo ya kuwekeza katika vijana.

Farid Ally alijiunga na Stanbic kupitia mpango wa mafunzo kwa wahitimu wa vyuo vikuu (Graduate Trainee Programme). Leo hii, anashikilia nafasi ya Mkuu wa Idara ya Masoko ya Fedha katika benki hiyo. Safari yake ni mfano wa namna kuwapa vijana nafasi za kujifunza, kupata uzoefu na kupewa majukumu kunavyoweza kuwaandaa kushika nafasi za juu za uongozi.

Mkutano huo uliofanyika kuanzia Jumanne, Novemba 3 hadi Ijumaa, Novemba 6, 2026, ulirejea barani Afrika kwa mara ya kwanza tangu ulipofanyika Johannesburg, Afrika Kusini, mwaka 2013. Uliwakutanisha vijana pamoja na viongozi wa biashara, watunga sera na watu mashuhuri kutoka mashirika zaidi ya 250 duniani.

Standard Bank Group, benki kubwa zaidi barani Afrika na benki mama ya Stanbic Bank Tanzania, ilishiriki kama mdhamini wa mkutano huo. Aidha, kundi hilo lilidhamini ushiriki wa vijana 61, wakiwamo wahitimu wa zamani na washiriki wa sasa wa mpango wake wa mafunzo kwa wahitimu wa vyuo vikuu.

Katika kundi hilo, wajumbe 30 walikuwa sehemu ya ujumbe maalumu uliojumuisha wahitimu na washiriki wa sasa wa programu hiyo kutoka maeneo mbalimbali, ikiwemo Afrika Mashariki. Ushiriki huo pia ulikuwa sehemu ya kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Wahitimu wa Standard Bank.

Akizungumzia uzoefu wake na safari ya kikazi, Farid Ally Mkuu wa Idara ya Masoko ya Fedha wa Stanbic Bank Tanzania, alisema:

“Nilijiunga na Stanbic kama mhitimu wa chuo kikuu kupitia mpango wa mafunzo, nikiwa na shahada na maswali mengi. Watu walionizunguka walinipa nafasi ya kujifunza, kufanya makosa na kupewa majukumu makubwa zaidi kila mwaka.

“Nilipokuwa Cape Town, nilikutana na vijana kutoka sehemu mbalimbali duniani wenye ari kama yangu. Nilirudi nikiwa na imani kuwa vijana wa Tanzania wanaweza kushindana na mtu yeyote duniani wanapopata mtu anayewaamini na kuwapa nafasi.”

Uwekezaji kwa vijana katika muktadha wa Tanzania

Ujumbe uliotolewa katika mkutano huo unaendana na umuhimu wa uwekezaji kwa vijana nchini Tanzania, ambako kundi hilo ni sehemu kubwa ya idadi ya watu na nguvu kazi ya taifa.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Tanzania ina watu milioni 21.3 wenye umri wa miaka 15 hadi 35, sawa na asilimia 34.5 ya watu wote nchini. Vijana wanachangia zaidi ya asilimia 55 ya nguvu kazi ya taifa.

Hata hivyo, ukosefu wa ajira kwa vijana bado ni changamoto, huku kiwango hicho kikiwa asilimia 9.5 kitaifa na kufikia asilimia 15.9 katika maeneo ya mijini, ambako wahitimu wengi hutafuta ajira zao za kwanza.

Serikali imewaweka vijana katikati ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na inalenga kutengeneza angalau ajira milioni 8.5 katika kipindi cha mwaka 2025 hadi 2030.

Akiwasilisha bajeti ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana kwa mwaka wa fedha 2026/27 bungeni, Waziri wa Nchi, Dk Joel Arthur Nanauka, alisema: “Serikali inawaona vijana si kama mzigo, bali kama rasilimali muhimu kwa maendeleo ya taifa.”

Kwa upande wake, Stanbic imejikita katika kuwaajiri vijana wa Kitanzania na kuwaendeleza kupitia programu zinazowapa nafasi ya kujifunza na kujenga uwezo wa kushika nafasi za uongozi.

Mpango wa mafunzo kwa wahitimu wa vyuo vikuu unawawezesha vijana kuanza kufanya kazi katika majukumu halisi ndani ya benki, huku wakipata nafasi ya kuzungushwa katika idara mbalimbali ili kuelewa kwa kina namna shughuli za benki zinavyoendeshwa.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa wakati wa mahafali ya programu hiyo mwaka 2024, asilimia 93 ya washiriki huendelea kubaki ndani ya benki. Wahitimu wa programu hiyo sasa wanashikilia nafasi mbalimbali ndani ya Stanbic na katika kampuni nyingine za Standard Bank Group.

Benki hiyo pia inaendesha programu ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, inayowapa fursa ya kupata uzoefu wa awali wa kufanya kazi katika sekta ya benki. Aidha, Chuo cha Mameneja wa Matawi (Branch Managers Academy) kimeanzishwa kwa ajili ya kuwaandaa wafanyakazi waliopo ndani ya benki kushika nafasi za uongozi wa matawi.

Akizungumzia mkakati huo, Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu, Rabina Masanja Rienks, alisema benki hiyo huwaajiri vijana kwa kuzingatia uwezo wao wa kukua na kufikia mafanikio ya baadaye, badala ya kuangalia tu maarifa waliyonayo wakati wa kuajiriwa.

“Tunawaajiri vijana wa Tanzania kwa kuangalia kile wanachoweza kuwa baadaye, si tu kile wanachokijua sasa. Wahitimu wetu huanza kufanya kazi halisi tangu wiki yao ya kwanza, huku viongozi wetu wakiwapa muda, mrejesho na majukumu.

“Safari ya Farid kutoka kuwa mhitimu wa mafunzo hadi kuwa Mkuu wa Idara ya Masoko ya fedha ndiyo mfano tunaoutoa kwa kila kundi jipya la wahitimu, kwa sababu inaonesha kuwa nafasi za juu za uongozi ndani ya benki hii ziko wazi kwao,” alisema.

Imani hiyo pia inashirikishwa na Standard Bank Group. Akizungumzia uwekezaji kwa vijana kabla ya mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa Kanda za Afrika na Shughuli za Nje ya Afrika wa Standard Bank, Lungisa Fuzile, alisema ukuaji na ustawi wa baadaye wa Afrika unategemea uwekezaji katika uwezo wa vijana wake.

Mwaka 2025, wahitimu 251 walijiunga na programu za mafunzo kwa wahitimu wa vyuo vikuu za Standard Bank Group katika nchi 11.

Akizungumzia mchango wa Stanbic katika maendeleo ya Tanzania, Rabina alisema benki hiyo imehudumia nchi kwa zaidi ya miongo mitatu na kwamba vijana wanaojiunga nayo leo ndio watakaokuwa sehemu ya uongozi wake katika miaka ijayo.

“Stanbic imehudumia Tanzania kwa zaidi ya miongo mitatu, na vijana wa Tanzania wanaojiunga nasi leo ndio watakaoiongoza benki hii katika miongo ijayo. Kuwekeza kwao ni namna ya kuwekeza katika nchi yetu. Tanzania ni nyumbani kwetu, na tunachochea ukuaji wake,” alisema.

Leave a Comment