
Msanii mkongwe wa Bongo Fleva, Sefu Shabani Ramadhan, maarufu kama Matonya, amefunguka kwa kina kuhusu mkasa wa kukamatwa kwake nchini Kenya mwaka 2026, akieleza mazingira yaliyopelekea kukutana na sakata lililogeuka kuwa moja ya nyakati ngumu zaidi katika maisha yake.
Katika mahojiano yake na Global TV Online katika kipindi cha Kontena, Matonya amesimulia kuwa safari yake nchini Kenya ilianza baada ya kwenda Tanga kumtembelea mama yake mzazi, kabla ya kukutana na marafiki zake wa Mombasa waliomwalika kwenda Watamu kwa ajili ya onesho la muziki.
Msanii huyo anasema onesho hilo lilifanyika vizuri na alikuwa akitarajia kurejea nyumbani akiwa amekamilisha shughuli yake, lakini mambo yalibadilika baada ya marafiki zake kumwalika kwenda kupata chakula cha jioni jijini Mombasa.

Kwa mujibu wa maelezo yake, baada ya chakula cha jioni, marafiki zake walipendekeza kuwaita wanawake wawili ili waungane nao katika burudani. Matonya anasema alimfahamu mmoja wa wanawake hao, lakini mwingine alikuwa akikutanana naye kwa mara ya kwanza siku hiyo.
Anadai kuwa baada ya burudani hiyo, hakumbuki vizuri kilichotokea, jambo lililofanya ashangae baadaye kujikuta katika kituo cha polisi cha Nyali.
Matonya anasema alielezwa kuwa kulikuwa na madai yaliyohusisha tukio lililotokea baada ya kundi hilo kubadilisha eneo walilokuwa, huku akidai kuwa alitaka kurejeshwa katika nyumba aliyokuwa akiishi.
Aprili 9, 2026, msanii huyo alifikishwa katika Mahakama ya Shanzu, Mombasa, akikabiliwa na mashtaka ya ubakaji, ambayo aliyakana.
Baada ya kufikishwa mahakamani, alikaa rumande katika Gereza la Shimo La Tewa kwa zaidi ya wiki mbili akisubiri kutimiza masharti ya dhamana ya shilingi 500,000 za Kenya. Pia alitakiwa kuwasilisha pasipoti yake mahakamani na kutoruhusiwa kuondoka nchini humo bila kibali cha mahakama.
Hata hivyo, Julai 2, 2026, mahakama ilimuachilia huru baada ya kumkuta hana hatia katika kesi hiyo.
Akizungumzia kipindi hicho, Matonya amesema kilikuwa miongoni mwa nyakati zenye maumivu makubwa katika maisha yake, akidai kuwa alihisi watu aliowaamini walimuweka katika mazingira yaliyomsababishia matatizo hayo.
Ameeleza pia kuwa sakata hilo liliathiri maisha yake binafsi na kazi yake ya muziki, akidai kupoteza takribani shilingi milioni tisa kutokana na mapato ya kazi zake za muziki kupitia majukwaa ya mtandaoni.
Mbali na athari hizo, amesema taarifa za kukamatwa kwake zilimuathiri mama yake mzazi kiafya, kwani ndugu zake walimweleza kuwa hali ya mama yake ilizorota kutokana na msongo wa mawazo kuhusu hatma ya mwanawe.
Matonya amesema tukio hilo limemfundisha kuwa makini zaidi katika kuchagua watu wa kuwaamini, akibainisha kuwa wakati mwingine watu unaowachukulia kuwa wa karibu wanaweza kuwa chanzo cha maumivu makubwa.
Pamoja na kurejea nyumbani, msanii huyo amesema maisha yake hayajarejea kama zamani, akieleza kuwa baadhi ya watu bado wanamtazama kwa mashaka kutokana na sakata hilo.