×

Equity Bank Yazindua Tawi la 20 Kigoma, Yafungua Fursa Mpya za Biashara na Uwekezaji

KIGOMA: Equity Bank Tanzania imezindua rasmi tawi lake la 20 mkoani Kigoma, hatua inayolenga kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha, kuchochea ukuaji wa biashara na kuongeza fursa za uwekezaji katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.

Uzinduzi wa tawi hilo umeongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dkt. Rashid Mohamed Chuachua, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mheshimiwa Balozi Simon Nyakoro Sirro.

Kufunguliwa kwa tawi hilo kunatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha huduma za kibenki kwa makundi mbalimbali ya wananchi, wakiwemo wafanyabiashara wadogo na wa kati, wakulima, wavuvi pamoja na wawekezaji wanaofanya shughuli za kiuchumi ndani na nje ya Tanzania.

Kupitia uwepo wake Kigoma, Equity Bank inalenga kutumia fursa za kibiashara zilizopo katika ukanda wa Ziwa Tanganyika, hususan biashara zinazounganisha Tanzania na nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Benki hiyo inatarajia kutoa huduma mbalimbali zitakazorahisisha shughuli za kifedha kwa wananchi na wafanyabiashara, ikiwemo huduma za kibenki, mifumo ya malipo ya kidijitali, ufadhili wa biashara na elimu ya fedha.

Huduma hizo zinalenga kuwawezesha wafanyabiashara kupata mitaji, kurahisisha miamala ya kifedha na kuongeza ushiriki wa wananchi katika uchumi rasmi.

Mbali na huduma za kibenki, Equity Bank pia inaunganisha shughuli zake za uwezeshaji wa kiuchumi na uhifadhi wa mazingira kupitia Mradi wa Uwezeshaji wa Kifedha na Uhifadhi wa Uchumi wa Buluu.

Mradi huo unalenga kuunganisha uwezeshaji wa jamii na juhudi za kuhifadhi Ziwa Tanganyika, ambalo ni rasilimali muhimu kwa shughuli za uvuvi, biashara na maisha ya wananchi wanaozunguka ziwa hilo.

Hatua hiyo inaweka msisitizo katika umuhimu wa kuendeleza shughuli za kiuchumi zinazozingatia matumizi endelevu ya rasilimali za majini na mazingira.

Kufunguliwa kwa tawi la Kigoma kunaongeza mtandao wa huduma za Equity Bank Tanzania na kuashiria dhamira ya benki hiyo ya kusogeza huduma za kifedha karibu zaidi na wananchi, huku ikilenga kuchangia maendeleo ya biashara na uchumi wa maeneo inayohudumia.

Kwa kaulimbiu yake ya “Tunawezesha Biashara, Tunafungua Fursa,” Equity Bank Kigoma inalenga kuwa sehemu ya safari ya kukuza biashara, uwekezaji na ujumuishi wa kifedha katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.

Leave a Comment