
Dar es Salaam, Novemba 18, 2026: Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania imeadhimisha kampeni yake ya ‘Mwaka wa Viwango’ kwa kushirikiana na washawishi (influencers) na watengeneza maudhui zaidi ya 100 katika hafla maalumu iliyofanyika Mikocheni, Dar es Salaam.
Hafla hiyo iliyobeba mandhari ya Kiswahili ilipambwa na burudani mbalimbali, zikiwemo muziki wa moja kwa moja na onesho la ngoma za Kigoma.
Wasanii G-Nako na Hamadai, waliohusika katika wimbo wa kampeni ya ‘Magifti ya Viwango’, walikuwa miongoni mwa waliowaburudisha wageni waliohudhuria hafla hiyo.

Katika mwaka huu, Yas imefanya kazi na washawishi 30 pamoja na watengeneza maudhui zaidi ya 100 kutoka maeneo mbalimbali nchini, wakitumia ubunifu wao kuwasilisha mada zinazohusu maisha ya kila siku, vichekesho, mtindo wa maisha, uwezeshaji wa vijana, ujasiriamali na maendeleo ya kidijitali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Christina Murimi, Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano wa Yas Tanzania, alisema watengeneza maudhui wamekuwa sehemu muhimu katika kusimulia hadithi zinazowafikia watu wengi na kuimarisha uhusiano kati ya chapa na jamii.
Aliongeza kuwa ‘Mwaka wa Viwango’ umejikita katika kuboresha ubora wa mtandao, huduma na fursa zinazotolewa kwa jamii, huku ushirikiano na wabunifu ukiwa sehemu ya safari hiyo.
Kwa upande wake, mtengeneza maudhui Willy Nkya alisema ushirikiano wake na Yas umempa nafasi ya kupanua ubunifu, kufikiri nje ya boksi na kutengeneza maudhui yanayounganisha malengo ya kampuni na utamaduni wa Kitanzania.
Kupitia hafla hiyo, Yas pia imeonyesha umuhimu wa kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa Kitanzania katika ulimwengu wa kidijitali, kwa kutumia mila na sanaa za asili kama sehemu ya usimulizi wa hadithi mtandaoni.
Yas imesema itaendelea kuunga mkono jamii ya wabunifu nchini kupitia ushirikiano, mafunzo na mipango mbalimbali inayolenga kukuza vipaji na kuimarisha sekta ya utengenezaji wa maudhui nchini.