
Wimbo wa Mvua Ya Baraka ulioimbwa na Zuchu akimshirikisha Diamond Platnumz umeendelea kufanya vizuri tangu ulipotoka, baada ya kufikisha watazamaji milioni sita (6) ndani ya wiki moja kwenye mtandao wa YouTube.
Mafanikio hayo yameendelea kuonesha mapokezi ya wimbo huo kwa mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva, huku sehemu ya maoni kwenye video hiyo ikijaa ujumbe wa pongezi, dua na mashabiki kutoka mataifa mbalimbali wakionesha namna walivyoupokea.
Baadhi ya mashabiki wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kuomba baraka katika maisha yao, wakiamini ujumbe wa wimbo huo unaendana na matumaini yao ya kupata mafanikio, furaha na maisha bora.
Mmoja wa mashabiki aliandika, “Mvua ya baraka itande kwako wewe unayesoma ujumbe huu, Amina,” huku mwingine akimuomba Mungu amfungulie milango ya kheri na baraka kila anayesoma maoni hayo.
Mbali na ujumbe wa baraka, mashabiki kutoka Kenya, Burundi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Nigeria na Ivory Coast wamejitokeza kuonesha upendo wao kwa wasanii hao.

Baadhi yao wamekuwa wakiomba kutambuliwa kupitia likes, huku wengine wakieleza kuwa wamekuwa wakiwafuatilia Diamond na Zuchu kwa muda mrefu lakini hawajawahi kupata alama nyingi za kupendwa kwenye maoni yao.
Wengine wameisifu video hiyo na kupongeza ushirikiano wa Diamond na Zuchu, wakieleza kuwa wasanii hao wamejitahidi katika kazi hiyo.
Pia, kuna mashabiki walioitumia nafasi hiyo kutoa maombi binafsi kwa Mungu, wakiomba wapate nyumba bora, maisha yenye unafuu na baraka kwa familia zao.
Kufikisha views milioni sita ndani ya siku saba ni hatua inayoongeza mafanikio ya wimbo huo, huku mwitikio wa mashabiki kutoka ndani na nje ya Afrika Mashariki ukiendelea kuonesha ukubwa wa usikivu wake.