
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka Wakuu wa Mikoa kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa kuweka mikakati madhubuti itakayoharakisha matumizi ya nishati hiyo katika maeneo yao.
Ametoa maelekezo hayo Novemba 28, 2026 jijini Dodoma, wakati wa Kikao Kazi cha Wakuu wa Mikoa kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, akisisitiza kuwa Wakuu wa Mikoa ni kiungo muhimu kati ya Serikali Kuu na wananchi, hivyo wanapaswa kusimamia ajenda hiyo kwa kushirikiana na wizara na taasisi mbalimbali, ikiwemo kuhakikisha taasisi za umma kama shule, vyuo na magereza zinatumia nishati safi ya kupikia.
Amesema licha ya hatua kubwa zilizopigwa na Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, bado kuna kazi kubwa ya kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanaitumia ili kupunguza athari za kiafya, kimazingira na kiuchumi zinazotokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Aidha, amewataka Wakuu wa Mikoa kufuatilia na kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa kuzindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Mei 8, 2024, kwa kupitia kila agizo na kuweka tathmini ya utekelezaji wake ili kuepuka maazimio yanayojirudia bila kutekelezwa.
Akitoa salamu za Wizara ya Nishati, Naibu Waziri, Mhe. Salome Makamba, amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034, wenye lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, huku matumizi hayo yakitarajiwa kufikia asilimia 35 ifikapo Desemba 2026.
Amewapongeza Wakuu wa Mikoa kwa juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kuwataka wadau wote kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza mkakati huo kwa lengo la kulinda afya za wananchi, kuhifadhi mazingira na kuboresha maisha yao.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Jossen Mramba, amesema matumizi ya nishati safi nchini yameongezeka kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia 28.6, huku Serikali ikilenga kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.

Amesema ongezeko hilo limetokana na juhudi za Serikali na wadau katika kusambaza majiko banifu 145,659 na mitungi ya gesi 484,410, hatua iliyochangia kupunguza vifo vinavyotokana na matumizi ya nishati isiyo safi kutoka 33,000 hadi 19,000 kwa mwaka.
Ameeleza kuwa Wakuu wa Mikoa wana nafasi muhimu katika kufanikisha mkakati huo kwa kuweka matumizi ya nishati safi kuwa kipaumbele, kuratibu wadau na kusimamia kampeni za uhamasishaji kwa wananchi ili kufikia lengo la Taifa la matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule, amesema wananchi wameendelea kuelewa umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, akieleza kuwa mwaka 2025 mkoa huo ulipokea mitungi ya gesi 19,530 yenye thamani ya Sh milioni 409 pamoja na majiko banifu 10,660 yenye thamani ya Sh milioni 505.8 kwa ajili ya wananchi.
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha matumizi ya nishati safi kupitia taasisi mbalimbali ikiwemo JKT na Jeshi la Magereza, huku akitangaza kuwa Mkoa wa Dodoma utaendesha zoezi la Nishati Safi Run Jumamosi ijayo kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia.
Wakuu wa Mikoa mbalimbali nchini wakiwa katika Kikao Kazi kuhusu Nishati Safi ya Kupikia kilichofanyika leo, Novemba 28, 2026, katika Ukumbi wa Hazina Square jijini Dodoma.
Kikao hicho kimeongozwa na kaulimbiu isemayo “Nishati Safi ya Kupikia, Okoa Maisha na Mazingira.”