Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini, DCP Mohamed Mpinga akizungumza jambo wakati alipozungumza na wanahabari leo.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya RSA Tanzania, Jackson Kalikumtima (katikati) akizungumza jambo kwa wanahabari (hawapo pichani).
Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani, ASP Deus Sokoni akifafanua jambo.
Na Denis Mtima/Gpl
NAIBU Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Hamadi Masauni anatarajia kuongoza kampeni ya kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kukabiliana na ajali Tanzania unaolenga kupunguza ajali hasa kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa mwaka ambapo watu wengi husafiri.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya RSA Tanzania, Jackson Kalikumtima alisema kuwa kampeni hiyo ni muda wa miezi sita na hasa italenga namna ya kukabiliana na ajali kwa kuchukua hatua stahiki bila ya kuwepo askari.
Alisema baada ya kufanyika uzinduzi wa kampeni hiyo hapo kesho, mabalozi wa usalama barabarani waliotawanyika kote nchini kwa kushirikiana na askari wa usalama barabarani, Sumatra na Chama Cha Kutetea Abiria (Chakua) na vyama vingine wataenda kwenye vituo vya mabasi, vyuoni, shuleni na kwa waendesha pikipiki kwa lengo la kutoa elimu juu ya usalama wa abiria katika chombo cha kusafiria na tahadhari yake.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, DCP Mohamed Mpinga alisema kuwa anawaomba wananchi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na vyama hivi au taasisi za kuangalia usalama wa abiria na kutoa taarifa mara moja wawapo kwenye chombo cha moto.
