
Wilbert Molandi |CHAMPIONI| Dar es Salaam
MSHAMBULIAJI wa kutegemewa wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma, amebadilishiwa hospitali akokuwa anamtibiwa Mikocheni na kuhamia London Health Hospital ili aiwahi mechi ya Simba. Mzimbabwe huyo, amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya goti aliyoyapata kwenye Michuano ya Kombe la Kagame kabla ya juzijuzi kurejea uwanjani katika mechi dhidi ya Mwadui FC na kujitonyesha.
Simba na Yanga zinatarajiwa kuvaana Februari 25, mwaka huu katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumatatu limezipata, mshambuliaji huyo amebadilishiwa hospitali kutokana na majeraha yake kushindwa kupona haraka. Mtoa taarifa huyo alisema, Mzimbabwe
huyo amepangiwa programu maalum ya matibabu ikiwemo kulifanyia masaji goti lake hilo ili kuhakikisha anapona haraka. “Ngoma anaendelea vizuri hivi sasa, kila siku anahudhuria kliniki inayomhitaji afike kila siku asubuhi kwa ajili ya matibabu hayo ya goti.
“Akiwa hospitalini hapo, amepangiwa programu mbalimbali za matibabu ikiwemo kulifanyia masaji goti lake na kufanyishwa mazoezi ya gym,” alisema mtoa taarifa huyo. Alipotafutwa Daktari Mkuu wa timu hiyo, Edward Bavo, alisema: “Ngoma anaendelea na matibabu kwenye Hospitali ya London Health yenye madaktari maalum wa magoti kutoka nchini India.
“Na maendeleo yake ni mazuri hivi sasa na hivi karibuni atarejea uwanjani mara baada ya kutoka Comoro kucheza mechi yetu ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Bavo. Licha ya kukosekana katika mechi kadhaa msimu huu, Ngoma tayari ana mabao nane kwenye Ligi Kuu Bara.