
Na OMARY MDOSE| CHAMPIONI JUMATANO| HABARI/ TANGAZO
BAADA ya kukosekana kwenye mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara, hatimaye nahodha wa Simba, Jonas Mkude, ameibuka na kufunguka hatma yake ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Mcameroon, Joseph Omog na msaidizi wake, Jackson Mayanja raia wa Uganda. Mkude ambaye hivi karibuni iliripotiwa alikuwa na mgogoro na viongozi wake, alishindwa kusafiri na timu hiyo ilipokwenda Songea kucheza mchezo wa ligi kuu dhidi ya Majimaji.
Baada ya kuukosa mchezo huo, wikiendi iliyopita pia Mkude aliishia kukaa benchi kwa dakika zote tisini pale walipoibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Kutokana na kiungo huyo mahiri kukosekana kwenye mechi mbili mfululizo huku akionekana kama hana umuhimu kwa jinsi matokeo waliyoyapata wakati yeye hayupo, ikaibuka hoja kwamba maisha ya Mkude ndani ya kikosi hicho yanaelekea ukingoni kwani mbadala wake, James Kotei anaweza kuziba pengo lake. Katika kuondoa utata huo, Mkude ameliambia Championi Jumatano kuwa:
“Ni kweli nimekosekana katika mechi hizo mbili lakini wenzangu wameipa timu matokeo mazuri, sikufanya makusudi kukosekana katika safari ya Songea, bali niliaga kutokana na matatizo ya kifamilia, na kila mmoja analijua hilo hapa.
“Ishu ya mimi kucheza au kutocheza ni jukumu la kocha na siwezi hata siku moja kulazimisha anipe nafasi ya kucheza, hivyo namuachia yeye ndiyo aamue kila kitu. “Inawezekana katika mchezo ambao sijacheza kocha ameona mimi sihitajiki siku hiyo ndiyo maana hakunichezesha, lakini siku ikitokea ananihitaji lazima tu nitacheza kwani hapa kikosini sina ugomvi na mtu yeyote yule.”
Kabla ya Mkude kukosekana kwenye michezo hiyo miwili ambayo Simba ilishinda kwa idadi mabao inayofanana, Mkude aliweza kucheza mechi 20 mfululizo tangu mwanzo mwa msimu huu ulipoanza Agosti, mwaka jana.