
Na Leah Marco| CHAMPIONI| Mwanza
SAFARI ya Yanga katika michuano ya Kombe la FA au Azam Sports Federation Cup (ASFC), imefikia tamati jana huku Mbao FC, vijana waliopanda daraja kwa ngekewa kucheza ligi kuu msimu huu, wakitia mchanga kwenye pilau la Jangwani.
Mbao waliopanda daraja wakichukua nafasi ya Geita Gold iliyoshushwa kutokana na skendo ya upangaji wa matokeo, wameonekana ni mwiba kwa wengi msimu huu na jana Yanga walikutana na dhoruba yao walipochapwa bao 1-0 na kuvuliwa ubingwa wao wa Kombe la FA kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa, huku wakiwaacha mashabiki wa Simba wakishangilia.
Hata hivyo, kipigo hicho cha Yanga kimezuia kwa muda uwezekano wa Simba kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao. Kama Yanga ingeshinda, Simba ingekata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa moja kwa moja.
Sasa Simba inachotakiwa kufanya ni kuhakikisha aidha inashinda taji la ligi kuu ishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ama ishinde Kombe la FA ili ishiriki Kombe la Shirikisho Afrika, au ishinde mataji yote ichague michuano ya kushiriki, halafu iiachie Mbao nafasi moja na Yanga iwe imetupwa nje.
Kwa Yanga kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, sasa inatakiwa ihakikishe inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Katika mchezo wa jana, bao pekee la Mbao lilifungwa na beki Andrew Vincent ‘Dante’ aliyejifunga katika dakika ya 27 wakati akiokoa mpira.
Yanga watajilaumu kwa kupata mipira mitano ya faulo nje ya eneo lao lakini wakashindwa kuitumia. Yanga walikosa nafasi kadhaa za wazi kupitia kwa Amissi Tambwe, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ lakini Mbao ndiyo walistahili kupata ushindi kutokana na soka walilolionyesha.
Baada ya mchezo huo, Cannavaro alisema: “Nawapongeza Mbao kwa ushindi, mpira haukuwa upande wetu leo (jana). Tumefungwa kwa bao la kujifunga lakini hatuna namna, inabidi tuangalie mechi za ligi sasa.”