×

Mbelgiji Ashusha Presha Yanga, Atupa Kombora Azam FC

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael, ameshusha presha ya mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaambia watulie kwa kuwa amejipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri dhidi ya Azam FC leo Jumamosi.

 

Eymael alikaribishwa kwenye Ligi Kuu Bara kwa fedheha baada ya kuchapwa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

 

Timu hizo zinatarajiwa kuvaana leo kwenye Uwanja wa Taifa mchezo utakaoanza saa 1 usiku na kutarajiwa kuwa na upinzani mkali, hiyo ni baada ya Yanga kutoka kwenye maumivu ya kipigo cha mabao 3-0 walichokipata dhidi ya Kagera Sugar.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Luc alisema anafahamu umuhimu na ugumu wa mchezao huo kutokana na ubora wa Azam katika ligi huku akiamini atapata matokeo mazuri katika mchezo huo.

 

Luc alisema katika mchezo na Kagera, alibaini upungufu ambao aliufanyia maboresho katika siku mbili, juzi Alhamisi na jana Ijumaa ili kuhakikisha anafanikisha malengo yake ya ushindi baada ya kutoka kufungwa na Kagera.

“Tulitakiwa tuimalize mechi yetu ya ligi na Kagera katika dakika za mwanzoni za kipindi cha kwanza, lakini umakini mdogo wa wachezaji wangu ukasababisha tufungwe, hivyo sitaki kitokee kile kilichotokea cha kushindwa kutumia nafasi hizo tulizokuwa tunazipata katika mchezo dhidi ya Azam.

 

“Niliona upungufu wa timu ambao ninaendelea kuufanyia marekebisho na kikubwa ni kuona timu inapata matokeo mazuri kwa kuanzia mchezo wetu dhidi ya Azam na hiyo inayofuata mbele yetu.

 

“Ninafahamu mashabiki wa Yanga wamekasirishwa na matokeo mabaya tuliyoyapata mchezo uliopita na Kagera, hivyo sitaki kuona mashabiki wakiendelea kuumizwa tena na matokeo, kikubwa waendelee kutusapoti, wasikate tamaa,” alisema Luc.

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Leave a Comment