
NAIBU Spika wa Bunge la Tanzania, Tulia Ackson, amemshukuru mke wa Rais Magufuli, Janeth Magufuli, kwa kuendelea kuwasaidia wananchi wenye uhitaji, wakiwemo watoto wenye ulemavu na wazee akitaja kitendo hicho kuwa ni cha kizalendo na chenye kutia moyo.

Tulia ametasema hayo leo wakati wa hafla fupi ya Mama Magufuli kukabidhi viti mwendo (Wheelchairs) vipatavyo 210 kwa baadhi waheshimiwa wabunge kwa ajili ya kuwagawia watoto wenye uhitaji majimboni kwao iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam.

Naibu Spika amesema kwamba katika kuwasaidia wazee na watoto wenye ulemavu Mama Magufuli amekuwa mfano wa kuigwa kwa wanawake kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii ya watu wenye mahitaji.

Mama Magufuli, ambaye ametoa msaada wa viti mwendo kwa watoto wenye ulemavu siku chache kabla ya Siku ya Wanawake Duniani, amewashukuru waheshimiwa Wabunge walioitikia mwito wake kupokea msaada huo.

“Kama mjuavyo kila tarehe 08/03 ya kila mwaka ni Siku ya Wanawake Duniani. hivyo basi nikiwa miongoni mwa wanawake nimeguswa na kuamua kusherehekea siku hii muhimu kwetu kwa kutoa zawadi ndogo ya viti mwendo kwa waheshimiwa wabunge ili wawafikishie wanangu wenye uhitaji kwenye majimbo yao kwa urahisi zaidi, kwani wao ndio wawakilishi wa wananchi”, alisema Mama Magufuli.
PICHA NA IKULU