UONGOZI wa Yanga rasmi umevunja kambi na kuwaruhusu wachezaji kurudi nyumbani kwao baada ya serikali kusitisha shughuli zote za michezo huku Kocha Mkuu Mbelgiji Luic Eymael akiwapa program za mazoezi wachezaji wote.
Hiyo, ikiwa ni siku chache tangu Serikali ya Tanzania kupitia kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kusimamisha michezo yote kwa muda wa siku 30 ili kupisha mlipuko wa Virusi vya Corona.
Yanga ilitarajiwa kuendelea na program yake ya mazoezi jana Alhamisi lakini hilo halikufanyika. Kati ya wachezaji ambao wako kwenye kikosi cha Yanga ni Bernard Morrison ambaye amekuwa kipenzi cha Wanajangwani baada ya kufunga bao pekee lililowapa ushindi dhidi ya Simba Machi 8, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela ni kuwa timu hiyo tangu mapema walichukua hatua jinsi ya kukabiliana na ugonjwa huo kabla ya serikali kutoa tamko.
Mwakalebela alisema kuwa wakati wachezaji wao wakiwa kwenye mapumziko, kocha Eymael ametoa program maalum za mazoezi kwa kila mchezaji kwa ajili ya kujiweka fiti ili ligi itakaporejea wawe tayari kwa mapambano.
Aliongeza kuwa program hizo za mazoezi watakazozifanya kwa muda wa siku 30, watazifanya gym na uwanjani kwa kukimbia mbio fupi na ndefu kwa wakati tofauti, lengo ni kuona watakaporejea uwanjani wanarejea na kasi waliyokuwa nayo awali.
“Mara kadhaa tumekuwa tukiona ligi ikisimama wachezaji wengi wanabweteka na kusihau kufanya mazoezi na kujikuta uzito kuongezeka na hiyo ni kutokana na kutofanya mazoezi.
“Kocha ameliona hilo na kuchukua maamuzi ya kuvunja kambi na kuwaruhusu wachezaji kurudi majumbani kwao ili kupisha tishio la Corona na mara serikali itakaporuhusu ligi kuendelea, basi haraka wachezaji wote wataingia kambini.
“Kambi tumeivunja kwa muda wa siku 30 ambazo Serikali ilitoa tamko la kusimamisha michezo yote ili kukwepa ugonjwa huo wa maambukizi ya njia ya hewa yanamalizika,” alisema Mwakalebela.
Stori na Wilbert Molandi, Dar es Salaam

