POLISI huko Kwale, Kenya, wanakisaka kikundi cha watu ambao wanadaiwa kumuua kijana Hezron Kotin eneo la Kibundani baada ya kumtuhumu kuwa na COVID-19.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Msambweni, Nehemia Bitok, alisema kijana huyo alikuwa akitoka kunywa pombe ambako kundi la vijana walianza kupiga kelele kuwa ana ugonjwa huo unaoenezwa na virusi vya Corona.
Vijana hao walishambulia mtu huyo wakiwa na silaha na kusababisha kifo chake. Bitok alisema waligundua jeraha kubwa kichwani mwake na kumkimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Msambweni.
Polisi wamewaonya raia dhidi ya kuchukua sheria mikononi au kutoa madai ya uongo wakati nchi inachukua hatua za kupambana na janga la COVID-19.
Kaunti ya Kwale imeanza kutoa mafunzo kwa maafisa wa afya juu ya kushughulikia kuenea kwa virusi hivyo. Afisa Mkuu wa Afya, Juma Mbete, alisema wametenga vituo vitano vya kushughulikia matukio ya ugonjwa huo katika kaunti zote tano.
