MENEJA wa mshambuliaji Reliant Lusajo wa klabu ya soka ya Namungo, Ahmad Kassim ‘Prezdaa’, amesema kuwa wapo tayari kufanya kazi na Yanga kama watamhitaji mchezaji wake ambaye amebakiza mkataba wa miezi mitatu tu na Namungo.
Lusajo amekuwa moto wa kuotea mbali msimu huu baada ya kuhusika katika mabao 14 ya Namungo akifunga mabao 11 na kutoa asisti tatu.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Ahmad Kassim alisema kuwa muda uliobaki kwenye mkataba wa Lusajo unawaruhusu kufanya mazungumzo na klabu yoyote.
“Lusajo amebakisha miezi mitatu kwenye mkataba wake na Namungo na nimekuwa nikipokea simu kutoka Yanga na Simba ili kuhitaji huduma yake, licha ya kuipa kipaumbele Namungo lakini tupo tayari kumalizana na yeyote atakayekuja mezani,” alisema Kassim.
Yanga inahusishwa na kuhitaji saini ya Lusajo ili kuziba pengo la mshambuliaji Yikpe Gnamien aliye kwenye hatari ya kuachwa baada ya kushindwa kuonyesha kiwango cha kuridhisha tangu ametua Jangwani katika usajili wa dirisha dogo la Januari.
Itakumbukwa kuwa Lusajo aliwahi kuichezea Yanga lakini aliachwa kutokana na kiwango chake kuwa chini, hata hivyo kiwango chake kimefufukia Namungo.
Joel Thomas, Dar es Salaam
