×

Kwa Nini Waliokatwa Mikia Waitese CCM?

WAKATI joto la uchaguzi mkuu likiendelea kupanda, baadhi ya mambo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yameanza kuibuka na kutengeneza matabaka ambayo hata Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyakemea.

 

Matabaka hayo tafsiri yake ni sawa na ubaguzi ambao Mwalimu Nyerere katika moja ya hotuba yake Machi 14 mwaka 1995 alisema; ‘’Dhambi ya ubaguzi kwa watu wa ndani ya taifa moja, dhambi hiyo haifi ni sawa na kula nyama ya mtu.”

 

Licha ya onyo hilo, matabaka hayo yamekuwa yakichochewa na baadhi ya makada wa chama hicho ambao sasa wanajiita CCM asilia, CCM wenyeji huku wale walioondoka na kurejea ndani ya chama hicho wakiitwa CCM B au wahamiaji.

 

Hakika ni majina ambayo yanapaswa kukemewa haraka na kuondoa tofauti hizo kwa njia za kidiplomasia ndani ya CCM ili kufuta sintofahamu iliyoibuka baina yao.

 

Utata huo umetokana na mwenendo wa kisiasa na kiutumishi ndani ya chama na serikali hasa baada ya kuwepo kwa wimbi la wapinzani kuhamia CCM.

 

Wimbi kubwa ambalo limekuwa likitajwa kuwa chanzo cha matabaka hayo ni baadhi ya wabunge waliohamia CCM kuteuliwa na kutetea nafasi zao walizokuwa nazo awali kule upinzani, vivyo hivyo kwa madiwani na mameya.

 

Kwa upande wa wabunge na madiwani, kelele zimekuwa nyingi hasa kwa WanaCCM hao asilia kushikilia msimamo wa Katiba ya chama hicho, kifungu cha 14(6) kinachompa mwanachama haki ya kupiga kura ya maoni kwa wagombea wa CCM wa nafasi za Udiwani wa Kata/Wadi, Ubunge na Uwakilishi wa Jimbo kwa kufuata masharti ya kanuni za CCM.

 

Asilimia kubwa ya hoja wanayotumia makada hao wa CCM, ni kitendo cha wabunge hao waliohamia CCM kutopigiwa kura za maoni. Hata hivyo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally aliwahi kuwaeleza waandishi wa habari kuwa kuna katiba mbili ndani ya chama hicho, katiba iliyoandikwa na isiyoandikwa.

 

Katiba iliyoandikwa inawapa haki wanachama hao kupiga kura za maoni kuchagua wabunge na madiwani, katiba isiyoandikwa ndiyo iliyotumiwa na Kamati Kuu kuwapitisha wagombea hao waliotoka upinzani.

 

Hii ina maana kuwa, Katiba hiyo ya CCM inatoa nguvu ya kimamlaka kwa Kamati Kuu ya chama kuamua mgombea wa nafasi hizo za ubunge na udiwani, ndio maana hata katika mchakato wa awali ndani ya chama kati ya wagombea watatu, aliyepata kura nyingi anaweza kuachwa na kupewa nafasi aliyeshika nafasi ya tatu.

 

Pamoja na hayo, wapo makada wa upinzani waliohamia CCM na kuteuliwa katika nafasi mbalimbali kama vile za mkuu wa wilaya, mkoa, katibu tawala na nyingine. Makada hao ni kama vile David Kafulila, Patrobas Kabambi na Julius Mtatiro.

 

Katika kuwatetea, Dk. Bashiru alisema makada hao ni sawa na vifaru kwa maana ya kuwa ni wachapa kazi wazuri, hivyo wamestahili kupewa nafasi.

 

“Na mwenyekiti amesisitiza hawa watu wapewe nafasi ili wakafanye kazi. Hawa ni vifaru na ukiteka kifaru lazima kiwe mstari wa mbele kwenye mapambano,” kauli hiyo ya Dk. Bashiru imeonekana dhahiri kuleta manung’uniko kwa baadhi ya makada wa chama hicho ambao wanaamini kuwa ndio wenye haki ya kupewa nafasi hizo kwa sababu tu walikipigania chama usiku na mchana tofauti na hao wanaoitwa ‘waliokatwa mikia’.

 

‘Waliokatwa mikia’ ni msemo ulioanzishwa Julai 23 mwaka 2016 na Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais John Magufuli wakati wa mkutano mkuu wa kumkabidhi kijiti cha uenyekiti kutoka kwa mtangulizi wake, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

 

Rais Magufuli alifananisha na ng’ombe waliokatwa mikia kuwa wakirudi zizini ni rahisi kuonekana huku ng’ombe wenzao wakiwashangaa.

 

Kwa mantiki hiyo, waliokatwa mikia ndani ya CCM sasa ni wengi, hakuna haja ya kuendelea kuvutana kwa sababu tu kwamba huyu ‘amekuja hastahili kupewa nafasi’, wanapaswa kujifunza kuwa hata wapinzani nao walinung’unika vivyo hivyo baada ya viongozi wao kuwapokea makada wa CCM.

 

Ni wazi kuwa wapo makada wa upinzani waliokasirika baada ya Agustine Mrema kuhamia NCCR Mageuzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 na kupewa nafasi ya kugombea urais, lakini alikiwezesha chama hicho kupata asilimia 28 ya kura.

 

Vivyo hivyo kwa Edward Lowassa, aliuwezesha muungano wa vyama vya upinzani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kupata asilimia 40 ya kura na wabunge wengi kiasi cha kuweka rekodi ya upinzani tofauti na miaka yote ambayo mgombea wa upinzani ametokana na wapinzani wenyewe na sio CCM.

 

Kwa mfano Dk. Wilbrod Slaa alipata asilimia 27 ya kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, hivyo kudhihirisha kuwa wanaotoka CCM pia wana nguvu na ni vifaru sawa na wanaotoka upinzani kuelekea CCM, vilevile ni vifaru ndio maana wanapewa nafasi.

 

Hakuna haja ya wanaCCM kuanza kunung’unika, watulie kwa sababu ndivyo karata za kisiasa zilivyo, aliye na uwezo anapewa nafasi. Kitendo cha kuanza kutibuana kama ilivyotokea kwa Mwita Waitara huko mkoani Mara, halileti picha nzuri kuelekea uchaguzi mkuu, jambo la msingi ni kutulia na kusubiri mchakato wa uchaguzi utakapotangazwa na kukubali matokeo.

Leave a Comment